Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRC na mageuzi safari za treni Dar

Treni Dar Mageuzii.png TRC na mageuzi safari za treni Dar

Thu, 9 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku moja baada ya gazeti la Mwananchi kuripoti juu ya hali mbaya ya usafiri wa treni jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amefanya ziara kusikiliza kero ya watumiaji wa usafiri huo.

Chalamila alidai ziara hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeona kupitia mitandao ya kijamii kipande cha video kinachoonyesha watu wakining’inia kwenye milango ya treni.

Shirika la Reli Tanzania (TRC), limeahidi kuongeza safari kutoka sita za sasa hadi nane ili kukabiliana na msongamano wa abiria. Akiwa ndani ya treni inayohudumiwa na TRC, Chalamila alianza ziara kituo cha Kamata Gerezani hadi Stesheni ya Pugu, ambako alizungumza na wananchi waliokuwa ndani ya treni.

Baadhi ya waliotoa kero zao, wameiomba Serikali kuongeza mabehewa au treni mbili zitoe huduma kwa wakati mmoja, na wametaka Jumamosi usafiri huo uwepo.

Mbali ya hilo, wameeleza kuna harufu ya ‘upigaji’ wa mapato katika ukatishaji wa tiketi za treni na huduma ya choo katika kituo cha Kamata kwa kuwa risiti hazitolewi.

Juzi gazeti hili lilizungumza na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra), iliyosema usafiri huo upo kwa miaka 10 sasa tangu ulipoanzishwa, lakini haujakidhi viwango vya usafiri wa mjini.

Malalamiko ya wananchi

Hemed Mussa, mkazi wa Gongo la Mboto aliomba siku za huduma ziongezwe, akisema, “Hii treni inatoa huduma Jumatatu hadi Ijumaa, Jumamosi pia sisi tunakwenda mjini kwa ajili ya shughuli zetu, tungeomba pia siku hii wananchi tuhudumiwe.”

Peter Lazaro, mkazi wa Pugu Bangulo, aliomba kuwe na treni mbili zitakazotoa huduma jioni ili kurahisisha usafirishaji.

“Watu ni wengi, wanaotoka Chanika, Mvuti na maeneo mengine wanaitegemea hii washuke hapa (Pugu Stesheni) wachukue magari, jioni ni shida sana watu wanahatarisha maisha yao wanapita madirishani,” alisema Lazaro.

Anna Jackson, mkazi wa Chanika alisema, “Sisi huwa tunalipa Sh1,200 kwa ajili ya kugeuza nalo na tumekubali ili tupate nafasi, lakini wanapofunga milango si sawa.”

Abiria mwingine, Martin Kingodi, alilalamikia kutozingatiwa kwa ratiba ya utoaji wa huduma, hivyo wamekuwa wakicheleweshwa katika shughuli zao.

Kwa upande wao, wanafunzi walisema mabehewa matatu yaliyotengwa kwa ajili yao hayatoshi na wanazuiwa kuingia kwenye mengine au kulipishwa nauli ya mtu mzima Sh600 badala ya Sh100 ya mwanafunzi.

Rajabu Athumani, alitilia shaka utaratibu wa urejeshaji tiketi kwa askari wanaosimama getini, akisema huenda tiketi hizo hutumiwa kwa mara ya pili, kwani kuna wakati wanapewa tiketi zilizochakaa.

Hoja ya aina hiyo pia iliibuka katika ukusanyaji wa mapato ya choo kilichopo ndani ya stesheni ya Kamata, baadhi ya wananchi wakihoji ni kwa nini hawapewi risiti.

Majibu ya TRC

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Amina Lumuli, aliyekuwapo kwenye ziara hiyo alisema kuwapo treni mbili ni ahadi isiyoweza kutekelezwa, lakini wanaweza kuangalia namna ya kuongeza behewa.

Kutokana na adha ya msongamano wa watu, alisema wanakwenda kuongeza idadi ya safari zinazofanywa kutoka sita kwa siku hadi nane, ili wananchi wapate huduma bora.

“Tungeomba wananchi muwe watulivu, lengo letu ni kuwahudumia na usalama wenu ni kipaumbele chetu, tutatangaza safari zitakazoongezwa zitakuwa ni za muda gani ili muweze kujua na kuzitumia,” alisema.

Akizungumzia kufunga milango, Amina alisema sheria inawataka waifunge treni inapotembea kwa ajili ya usalama. Kuhusu wanafunzi alisema wametengewa mabehewa manne, pia lipo kwa ajili ya wazee lakini kutokana na wingi wa watu utaratibu umekuwa haufuatwi.

Akifafanua juu ya ukusanyaji wa tiketi, alisema hilo linafanyika kutokana na baadhi ya wananchi wasio waaminifu hutumia moja kwa safari nyingine.

Pia aliahidi kufuatilia na kufanyia kazi malalamiko kuhusu kutotolewa risiti kwa huduma ya choo.

Mkuu wa Mkoa

Chalamila aliahidi watakwenda kufanyia kazi kero zilizotolewa na wananchi, akisema Serikali inatambua treni kama usafiri wa haraka kwa sasa kutokana na ujenzi wa barabara ya mwendokasi unaondelea kwenye Barabara ya Nyerere.

Ujenzi huo unaoishia Gongo la Mboto kutoka mjini unatajwa kusababisha foleni inayofanya watu kutumia muda mrefu barabarani, hivyo wengi kuhamia kwenye treni.

Mbali ya hilo, alisema wanafahamu kuwa eneo la Banana hadi Ukonga Gerezani magari mengi yanapishana katika njia moja hivyo kuwa na usumbufu.

Alisema makubaliano yaliyopo ni mkandarasi kuongeza njia nyingine ili magari yapishane kama ilivyokuwa awali.

“Lengo ni kupunguza foleni na kusaidia watu wawahi kazini. Si kujenga bila kuweka njia mbadala,” alisema Chalamila.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live