Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRC kupeleka abiria 2,000 kaskazini kwa siku

760f4e24fa79bef21d323ac50c32b887.png TRC kupeleka abiria 2,000 kaskazini kwa siku

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KUTOKANA na ongezeko la abiria hususani katika kipindi hiki cha sikukuu za mwishoni mwa mwaka, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limejipanga kuongeza safari za treni zinazokwenda katika mikoa ya Kaskazini ikiwemo kuongeza idadi ya mabehewa.

Akizungumza na HabariLEO kwa njia ya simu juzi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha shirika hilo, Jamila Mabrouk alisema kutokana na wingi huo wa abiria kipindi hiki cha sikukuu shirika hilo limeongeza mabehewa kutoka nane yaliyokuwepo hadi 15.

Aidha alisema kwamba behewa moja lina uwezo wa kubeba watu 120. Kwa maana hiyo safari moja inabeba mpaka ya abiria 2,000 kutokana na wengine kupanda na kushuka njiani.

“ Kuanzia Oktoba mwaka huu, tuliona wateja wanaongezeka hivyo tukaongeza safari kutoka nne kwa wiki hadi safari sita, lengo ni kuhakikisha msimu huu wa sikukuu tunatoa huduma bora kwa wananchi,” alieleza.

Treni hiyo ya Kaskazini inatokea Dar es Salaam kwenda na kurudi kupitia mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

Aidha, shirika hilo pia limesema limeanzisha huduma ya ukataji tiketi kwa njia ya mtandao ili kuwarahisishia abiria na kuwapunguzia adha ya kurundikana kwenye foleni wakisubiri kukata tiketi. Mteja atatakiwa kuingia tovuti ya shirika hilo ambayo ni www.trc.co.tz na kukata tiketi hiyo popote alipo

Alisema kutokana na ongezeko hilo la safari sasa treni hiyo itakuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Arusha kuanzia siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam siku za Jumanne, Alhamisi na Jumamosi.

Alisema awali treni hiyo ya Kaskazini ilikuwa na safari nne ambazo kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha ilikuwa ni Jumatatu na Ijumaa na kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam ilikuwa ni Jumanne na Alhamisi.

Aliongeza kuwa pamoja na mabadiliko hayo ya kuongeza safari na mabehewa shirika hilo litaendelea kubadilika kulingana na mahitaji.

Treni ya Dar es Salaam- Moshi ilirejesha safari zake katika mikoa ya Kaskazini Desemba 6 mwaka jana, ikiwa ni miaka 25 tangu ilipositisha safari mwaka 1994.

Mafanikio ya usafi huo wa treni ya Dar es Salaam-Moshi, yalianza kuonekana mwaka jana baada ya kusafirisha wastani wa abiria 7,800 na kukusanya zaidi ya Sh milioni 140 kwa siku 21 ambapo mwaka huu, mafanikio hayo yanatarajiwa kuongezeka.

Chanzo: habarileo.co.tz