Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRC kuja na reli katikati ya majiji

Kadogosa1 Relili TRC kuja na reli katikati ya majiji

Fri, 8 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirika la Reli Tanzania (TRC) linafanya utafiti wa kuwa na reli katikati ya majiji likiwamo la Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma na kuziunganisha na viwanja vya ndege.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema mwishoni mwa Agosti, mwaka huu treni ya mkandarasi inayotumia dizeli itaanza majaribio kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma baada ya kukamilika kwa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro kwa asilimia 97.

Kadogosa aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa nia ya shirika hilo kujenga reli katikati ya miji na majiji ni kutokana na ongezeko la watu. Alisema ujenzi wa reli hizo utahitaji ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi na maandalizi ya kutafuta watu kujenga yanaendelea.

“Kwenye kituo kikuu cha reli kutakuwa na kituo cha mabasi ya mwendo kasi ambacho kitatumika baada ya abiria wanaoshuka na kwenda maeneo mbalimbali ndani ya jiji husuka. Tunaendelea na utafiti kuona namna ya kujenga reli itakayokwenda Uwanja wa Ndege, Kigamboni na Mwenge hadi Tegeta (Dar es Salaam),” alisema Kadogosa.

Alisema ujenzi wa reli ya treni kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza unaendelea vizuri. “Rais aliahidi kuendeleza miradi yote iliyoanzishwa, hili ni jambo gumu kwa sababu lazima awe na fedha za kutosha kwani pamoja na kujenga barabara, reli na vingine, huduma za afya, elimu bado vinaendelea, hivyo tunaomba wananchi muwe na imani kwamba kila kitu kitamalizika,” alisema Kadogosa.

Alisema baada ya kukamilika kwa reli ya SGR, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) itakuwa na jukumu la kupanga bei ya nauli na kuthibitisha kama ni salama. “Hatuwezi kubeba abiria mpaka mamlaka inayotusimamia itakapojiridhisha, hivyo hatuwezi kusema ni lini watu wataanza kutumia treni hiyo,” alisema Kadogosa.

Alisema reli hiyo itaunganisha Dar es Salaam, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hivyo katika miaka mitano ijayo wanatarajia kuunganisha reli hiyo na miji mikuu ya Congo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live