Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamefanya makabidhiano ya boti za doria na kampuni ya Amikan Ventures katika kituo cha forodha cha TRA Jijini Dares Salaam ambapo boti mbili zimekabidhiwa na kuzinduliwa kwa ajili ya kuanza kazi.
Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata amesema boti hizo zitafanya kazi ya doria katika Pwani ya Tanzania na maziwa kupambana na vitendo vya magendo ambavyo vinahatarisha mipango ya TRA katika kukusanya mapato ya Nchi.
Amesema Waingizaji wa bidhaa bandia na bidhaa za magendo wamekuwa wakitumia mwanya wa urefu wa mpaka wa Pwani ya Bahari ya Hindi kwa kuingiza bidhaa bandia ikijumuisha dawa, vyakula, mavazi, viatu, vifaa vya elektroniki, na vinywaji vyenye pombe.
"Uingizaji wa bidhaa kama hizi zinaathiri vibaya uchumi wa Nchi kupitia kukosa mapato, kukwamisha ukuaji wa viwanda vya ndani na biashara halali, na kuathiri afya na usalama wa Watumiajiā€¯
Aidha amesema gharama za ununuzi ya boti hizo zilipitishwa wakati wa bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 ambapo Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ilitenga bajeti ya Tsh 2.5 Billioni kwa ajili ya ununuzi wa boti mpya za doria, hivyo boti hizo mbili ambazo wamekabidhi wameona wazipeleke zikafanye kazi za doria kwa mikoa ya Dar es salaam na Kigoma ambapo kuna matukio mengi ya magendo.