Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yawatahadharisha walipa kodi dhidi ya matapeli

46536 Pic+tra.png

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewatahadharisha walipa kodi kuhusu uwepo wa watu wanaotumia jina la mamlaka hiyo kufanya utapeli.

Tahadhari hiyo imetolewa leo Jumatano Machi 13, 2019 na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo wakati akizungumza na walipa kodi katika ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam.

Amesema matapeli hao hupiga simu kwa wafanyabiashara na kujitambulisha ni maofisa wa TRA wakiwaeleza wanajiandaa kwenda kukagua ulipaji wao wa kodi.

“Wakati mwingine wanatoa maelekezo ya kupewa fedha ili wasifike eneo husika, huu ni utapeli tunaomba wafanyabiashara wawe makini. TRA hatuna utaratibu wa kuwapigia simu na maofisa wetu wanapofika eneo lolote wanakuwa na vitambulisho,” amesema.

Kayombo pia amewasisitiza wafanya biashara kulipa kodi ya mapato ya robo mwaka kwa wakati kabla ya kupita kwa tarehe ya mwisho ambayo ni Machi 30, 2019 ili kuepusha usumbufu.

Amesema kodi hiyo ikilipwa kwa wakati itaondoa uwezekano wa kutokea msongamano ambao kwa kiasi kikubwa huchangia mfumo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

“Watu wakiwahi kulipa kodi hata vituoni kutakuwa hakuna msongamano, wakisubiri mwisho lolote linaweza kutokea ikiwemo mfumo kushindwa kufanya kazi, matokeo yake unapitisha muda na hatimaye unatozwa faini,” amesema.

“Suala la muda lizingatiwe pia kwenye kodi ya majengo, tunaona Bunge limepunguza kiwango cha kodi hivyo hakuna sababu ya watu kuchelewesha na kusubiri dakika za mwisho, tulifanye suala la ulipaji kodi kuwa utamaduni wetu,” ameongeza.



Chanzo: mwananchi.co.tz