Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yawahimiza abiria tiketi mtandao

Tiketi Pic Data.png TRA yawahimiza abiria tiketi mtandao

Sun, 19 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewahimiza abiria wa safari ndefu kutumia mfumo wa ukataji tiketi za mabasi kwa njia ya mtandao ikisema una faida pana kwao na kwa sekta nzima ya usafirishaji.

Faida hizo ni pamoja na kuondoa usumbufu wa abiria kwenda vituoni kukata tiketi kwani unamuwezesha kupata huduma hiyo akiwa sehemu yeyote yenye mtandao nchini.

Mfumo huo pia unawaepusha abiria na usumbufu wa wapiga debe waliopo katika vituo au stendi za mabasi na unawaepusha na ulanguzi wa tiketi au kupanda kwa nauli hususani wakati wa likizo za wanafuzi na sherehe za mwisho wa mwaka.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Shabani Salim alisema ili mpango huo ulioanza kutekelezwa Julai mwaka jana ufanikiwe mamlaka yao inaendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa mabasi.

“Leo tumekutana hapa Iringa na wamiliki wa mabasi ya abiria waliopo mkoani kwetu Iringa kwa lengo lile lile la kufikisha zaidi elimu kuhusu mfumo huu, jinsi unavyofanya kazi na faida zake ikiwemo serikali kupata mapato yake sahihi,” alisema.

Alisema wapo watoa huduma wachache waliounganisha mfumo wao na TRA na kwa ambao bado wanatakiwa kujiunga ili taarifa zote za tiketi zinazokatwa zionekane katika mamlaka hiyo kwa lengo la kufuatilia mapato yanayotokana na huduma ya usafirishaji.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Upendo Coach inayofanya safari zake kati ya Iringa na Dar es Salaam, Charles Nyagawa aliipongeza serikali kwa kuja na mfumo huo akisema utawasaidia kwa kiwango kikubwa kuyanusuru mapato yao yaliyokuwa yakichotwa na wapiga debe.

“Kuna wakati mpiga debe anamkatia tiketi abiria kwa Sh 25,000 kutoka Iringa kwenda Dar es Salaam lakini kwa kisingizio kwamba yeye ndiye kamtafuta abiria huyo anachukua Sh 7,000 mmiliki anaachiwa Sh 18,000,” alisema.

Kimahesabu alisema kiwango hicho ni kikubwa na kinampa maumivu mmiliki kwasababu mbali na kulipa kodi mbalimbali za serikali kwa kutoa huduma hiyo ya usafirishaji, anatakiwa kuwalipa wafanyakazi, mafuta na matengenezo ya basi lenyewe.

Kwa upande wake Meneja wa Tiketi Mtandao kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Thadei Mtui alisema tiketi mtandao zinafaida kubwa kwa wamiliki wa mabasi kwani zinawanusuru na upotevu wa fedha zinazochukuliwa na wapiga debe kwa kisingizio cha kutafuta abiria.

“Mfumo huo wa tiketi mtandao umewasaidia kwa kiasi kikubwa wamiliki wa mabasi na kuzuia mianya ya upotevu wa mapato pamoja na fedha ambazo walipaswa kupata wao lakini awali ziliku zikienda moja kwa moja kwa wapiga debe,” alisema.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA) mkoa wa Iringa, Mohamed Ally ameishukuru TRA kwa kuwashirikishwa kwenye kikao hicho na akasisitiza suala la utoaji wa elimu kuhusu Tiketi Mtandao kwa watumiaji lakini pia kwa baadhi ya wasafirishaji ambao bado hawajaanza kutoa huduma hiyo ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.

“Mfumo wa Tiketi Mtandao una umuhimu na faida kubwa ikiwemo kuokoa muda ambao abiria anatumia wakati wa kwenda kukata tiketi katika ofisi za mabasi, kuepuka changamoto za wapiga debe lakini pia husaidia abiria kupata stahiki zake endapo itatokea ajali au madhara yoyote kwa kupewa fidia na bima,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live