Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yavuka lengo makusanyo Machi 2022 ikikabiliwa na ‘mlima’ wa robo ya nne

Wafanyabiasharapic Data Imesalia miezi mitatu mwaka wa fedha umalizike

Mon, 4 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ikiwa imesalia miezi mitatu kumalizika kwa mwaka wa fedha wa 2021/22, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema imekusanya Sh16.69 trilioni katika robo tatu za awali ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.8 kutoka kwenye mapato yaliyokusanywa kipindi kama hicho mwaka 2020/21 huku ikivuka lengo la makusanyo mwezi Machi.

Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 TRA ilikusanya Sh13.59 trilioni, kiwango ambacho ni chini kwa Sh3.1 trilioni ikilinganishwa na mapato ya robo tatu za awali katika mwaka huu wa fedha unaoishia Juni 30.

Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidato ameeleza kwenye taarifa kwa umma leo (Aprili 3, 2022) kuwa kiwango hicho kilichokusanywa na TRA katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022 ni sawa na asilimia 97.3 ya lengo la kukusanya Sh17.15 trilioni.

Kidata amesema katika kipindi cha Machi 2022 pekee mamlaka hiyo imevuka lengo la kukusanya kodi ya Sh1.98 trilioni baada ya kukusanya kodi ya 2.06 trilioni ikiwa ni ufanisi wa asilimia 103.6.

Mapato yaliyokusanywa Machi 2022 ni makubwa zaidi kwa asilimia 23.17 ikilinganishwa na kiwango cha kodi kilichopatikana kipindi kama hicho mwaka jana ambapo Serikali ilikusanya Sh1.67 trilioni.

“Makusanyo haya kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na kuongezeka kwa uhiari wa kulipa kodi, kuimarika kwa mahusiano ya TRA na walipa kodi kunakochagizwa na utatuzi wa migogoro nje ya mahakama pamoja na kushughulikia malalamiko ya walipa kodi kwa wakati,” amesema Kidata.

Sanjari na hayo, bosi huyo wa TRA amesema mafanikio hayo pia yamechagizwa na kuimarika kwa uzalishaji wa viwanda vya ndani na biashara za kimataifa.

Pamoja na mafanikio hayo, Kidata na timu yake watakuwa na kibarua cha kukusanya 5.49 trilioni kwa miezi mitatu iliyosalia ili kuweza kutimiza malengo ya mapato ya kodi katika mwaka wa fedha wa 2021/22 ya Sh22.18 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 13.5 ya Pato la Taifa.

Ili kutimiza lengo hilo itatakiwa kukusanya kwa angalau wastani wa Sh1.83 trilioni kwa mwezi kati ya Aprili na Juni 2022, kiwango ambacho ni chini kidogo na kilichokusanywa Machi 2022.

Tanzania imepanga kukusanya na kutumia Sh37.9 trilioni katika mwaka wa fedha wa 2021/22 unaoishia Juni 30 huku asilimia 37 ya mapato yote yakitumika katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Katika kuendeleza mafanikio hayo, Kidata amesema mamlaka hiyo imepanga kutekeleza mipango mbalimbali ikiwemo kuanza rasmi kutumia mfumo ulioboreshwa wa kielektroniki wa uwasilishaji wa ritani za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuanzia Apili na kuongeza usimamizi, ufuatiliaji na uhamasishaji wa kutoa na kudai risiti za kielektroniki za EFD.

Tangu ameingia madarakani Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akizitaka taasisi za umma kama TRA kutengeneza mazingira rafiki kwa ukuaji wa biashara ikiwemo kuacha kuwabambikizia kodi wafanyabiashara au kufungia biashara zao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live