Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yatoa maagizo mengine kwa wafanyabiashara

322c4e22fa02eaf43bdd75079e0ff7f4 TRA yatoa maagizo mengine kwa wafanyabiashara

Mon, 14 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wafanyabiashara wadogo mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuacha kuingiza bidhaa za magendo kupitia njia zisizo halali ili kuepuka madhara ya kiafya kwa jamii na kiuchumi kwa taifa.

Wito huo ulitolewa na Ofisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Odupoi Papaa wakati wa utoaji elimu kwa wafanyabiashara wa mipakani kuhusu athari za biashara za magendo katika mpaka wa Kenya na Tanzania wa Holili.

Alisema madhara ya bidhaa hizo yameanishwa katika maeneo matatu ikiwamo afya ya walaji kutokana na uwezekano wa kutumia bidhaa zisizo na ubora na ambazo zimeisha muda wake wa matumizi.

"Kuna baadhi ya watu ambao wanabadilisha bidhaa kwenye mifuko mipya wakati zimekwisha muda wa matumizi na kusababisha madhara makubwa kwenye afya zetu, hivyo tukatae bidhaa za magendo. Madhara mengine yanayopatikana ni kwa nyinyi wenyewe kukamatwa na bidhaa za magendo ambapo madhara yake ni makubwa ikiwamo kupigwa faini na kufungwa jela,” alisema Papaa.

Kwa upande wake, Ofisa Mfawidhi Kituo cha Forodha Holili, Yusuph Mwahu aliwashauri wafanyabiashara wadogo kupitia lango kuu kwani barabara ipo vizuri na ushuru upo vizuri na wameweka dirisha maalumu kwa ajili ya kulipa ushuru kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Aliwataka wafanyabiashara kutopita maporini kwa lengo la kukwepa kodi kwa kupitisha bidhaa za magendo, bali wapite lango kuu la Holili.

Pia alikitaka kitengo cha elimu kwa mlipa kodi cha TRA kuendelea kutoa elimu mara kwa mara hasa sehemu za mipakani ili uwelewa juu ya umuhimu wa kulipa kodi uwe mkubwa zaidi kwa jamii.

Mkazi wa Holili, Abdul Abdul ambaye awali alikua akifanya biashara ya magendo, alisema ameacha kazi hiyo na anapita katika lango kuu na kuwataka maofisa wa TRA waendelee kutoa elimu ili watu wengi wawe na uelewa kuhusu athari za kupitisha bidhaa za magendo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live