Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yatoa elimu athari za magendo

A7a1f7a3659d166a2ea5162f9dc1795f TRA yatoa elimu athari za magendo

Wed, 16 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewaelimisha wananchi na wafanyabiashara kuhusu athari za magendo.

Mamlaka hiyo imesema licha ya kuikosesha serikali mapato, bidhaa za magendo pia zinaweza kuhatarisha afya za walaji.

Akizungumza wakati wa kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Mara, Ofisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa TRA, Stephen Kauzeni alisema ni muhimu wafanyabiashara wakapitisha bidhaa katika njia rasmi ili kuhakikisha kila inayoingia nchini inakaguliwa ubora wake kwa lengo la kulinda afya za walaji.

“Athari nyingine ya magendo ni nchi kukosa takwimu sahihi za bidhaa zinazoingia na kutoka nchini, kukosekana kwa ushindani sawia wa wafanyabiashara kutokana na wengine kuuza bei za juu kwa sababu wamelipia ushuru na wengine kuuza bei za chini kutokana na kupitisha bidhaa kwenye njia zisizo rasmi,” alisema.

Ofisa Msimamizi wa Kodi wa TRA, Julieth Kidemi alisema serikali inategemea kodi ili iweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi kwa kupitisha bidhaa kwenye njia zisizo rasmi wanaichelewesha nchi kupiga hatua.

“Kupitia kodi tunazolipa nchi yetu inajenga miundombinu ya reli, barabara, inalipa mishahara ya watumishi, inajenga shule na mambo mengine kama hayo, hivyo nawasihi tuache magendo na tulipe kodi kwa hiari,” alisema.

Nao wakazi wanaoishi eneo la Mtimrabu ambalo ni mpakani mwa Tanzania na Kenya, waliomba TRA kujenga ofisi katika eneo hilo ili waweze kupata huduma za forodha na kuondoa usumbufu wa kufuata huduma hizo katika mpaka wa Sirari.

“Tumefurahi sana kutembelewa na maofisa wa TRA ambao wametupatia elimu juu athari za magendo, lakini sisi wakazi wa hapa Mtimrabu tunaiomba serikali itujengee ofisi ya TRA maana tunahangaika sana kufuata huduma za forodha Sirari,” alisema Paulo Moti.

Mwananchi mwingine, Mwita Juma alisema kutokuwapo kwa ofisi ya TRA katika eneo hilo kunachochea watu wengi kufanya magendo na kusababisha serikali kukosa mapato.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango mkoani Mara ilianza Februari 7, mwaka huu na itamalizika Februari 21, mwaka huu, ambapo baada ya kumalizika katika Wilaya ya Tarime, maofisa wa TRA wataelekea Wilaya ya Bunda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live