Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yashinda tuzo uandaaji wa mahesabu

TRA MAHESABU TRA yashinda tuzo uandaaji wa mahesabu

Fri, 2 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imeshinda tuzo ya jumla ya uandaaji wa mahesabu katika taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali ambazo zinatengeneza mahesabu yake katika utaratibu wa kimataifa ujulikanao kama ‘International Public Sector Accounting Standards’ (IPSAS)

Aidha mamlaka hiyo imeshinda nafasi ya kwanza ya uandaaji wa mahesabu kwenye taasisi za serikali kwa mwaka 2021.

Naibu Kamishna Upelelezi wa Kodi wa TRA, Robert Manyama ameeleza hayo baada ya kupokea tuzo katika Kituo cha Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).

Akielezea siri ya ushindi huo amesema ni ueledi katika kutekeleza miongozo iliyowekwa ya uandaaji wa mahesabu inayofuatwa na mamlaka hiyo.

“Tunafurahia ushindi huu kwa sababu inatuongezea hali ya kuaminika. Sisi kama chombo cha umma tunapoonyesha kuwa tunatoa hesabu zetu sawa sawa basi umma unatuamini kwamba tunafanya kazi sawa sawa.

“Ni vizuri kwa taasisi nyingine za serikali kushiriki ili kujiongezea kuaminika katika utendaji wa shughuli zao hasa sisi ambao tunafanya kazi kwa niaba ya wananchi ni vema sana kutumia chombo kama hiki chenye wataalam wanaoweza kuonyesha utendaji wetu upo namna gani,”amesema.

Amesema kwa kuonyesha utendaji wao kuwa safi itawafanya waaminike na wananchi kwa kuwa wanajua chombo chao kinafanya kazi sawa sawa. Amewataka walipa kodi walipe kodi inavyostahili ili TRA iendelea kutoa huduma bora kwao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania, Profesa Sylvia Shayo Temu amesema bodi imezingatia viwango vya kimataifa ambavyo vinatoa uhitaji wa kuonyesha mambo mbalimbali ambayo ni lazima yaonyeshwe kwenye taarifa ya hesabu.

Ametolea mfano wa taasisi ya serikali ya TRA kuwa imekuwa wazi katika taarifa zake, hivyo inawapa moyo walipa kodi kwamba fedha za wananchi wanazopokea ni salama zinapelekwa serikalini kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa.

Pia zinakusanywa kwa taratibu na kuandikwa kwa viwango na taratibu zinazozingatia sheria na miongozo mingine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live