Tanga. Uingizaji wa bidhaa za magendo unaendelea kuwa tatizo sugu mkoani Tanga, licha ya vyombo mbalimbali vya dola kuimarisha doria baharini na njia nyingine za panya.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Mkoa wa Tanga, Thomas Masese ametoa taarifa hiyo leo wakati wa utoaji wa tuzo kwa walipakodi bora wa mkoani hapa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23.
Amesema bado wapo wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiingiza nchini bidhaa kwa kupitia njia za panya za nchi kavu na baharini kupitia bandari bubu zilizopo mwambao wa Hahari ya Hindi.
"Bidhaa ambazo bado zinaingizwa kwa kwa njia za magendo kwa mujibu wa Masese ni sukari, mafuta ya kupikia na kanga," amesema Masese.
Amesema katika kupambana na uingizaji wa bidhaa za magendo, Serikali imepeleka Mkoa wa Tanga boti ya kisasa ya kuimarisha doria baharini na pia msako wa katika njia za panya za kupitia mipaka na nchi jirani imeimarishwa zaidi.
Mapato
Kwa upande wa ukusanyaji mapato,Meneja huyo amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Mkoa wa Tanga ulikusanya Sh214.39 bilioni kati ya lengo la Sh232.64 bilioni sawa na asilimia 92 ikiwani ongezeko la Sh43.53 bilioni ikilinganishwa na makusanyo ya Sh170,86 bilioni ya mwaka 2021/22 ambayo ni ukuajji wa asilimia 20.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Maulid Sulumbu amesema Serikali haiwezi kuwafumbia macho wanaofanya magendo bali itawakamata wote na kuwafilisi kwa kuwa huko ni kurejesha nyuma maendeleo ya nchi.
Aliyepata tuzo ya mshindi wa jumla ya mlipakodi mkubwa ni Tanga Pharmaucetical and Plastic Ltd kampuni iliyopo jijini Tanga ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo.