Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yaita walipakodi kabla Juni 30

TRA.webp TRA yaita walipakodi kabla Juni 30

Tue, 16 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka wafanyabiashara na walipakodi wote kuwahi kulipa kodi zao za awamu ya pili, pamoja na malimbikizo yote kabla ya Juni 30, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, aliyasema hayo alipokuwa anazungumza na walipakodi wa mkoa wa Lindi.

Aliwashauri walipakodi kutosubiri kulipa kodi zao tarehe ya mwisho ili kuepuka msongamano kitu ambacho kinaweza kusababisha usumbufu kwao na maofisa wa TRA.

"Lakini tunaomba walipakodi wetu wazingatie kuwa misongamano ni hatari hasa kwa kipindi hiki dunia inapopambana na janga la corona," alisema Kayombo.

Aidha, aliwakumbusha wamiliki wa majengo kulipa kodi zao mapema kuepuka adhabu ya kuchelewa kulipa na kusababisha usumbufu kwao.

Alisema kwa sasa viwango vya kodi ya majengo vimekuwa rafiki na kwamba kwa nyumba ya kawaida isiyo ya ghorofa ni Sh. 10,000 na ya ghorofa ni Sh. 50,000 kwa kila sakafu kwa nyumba zilizopo katika Jiji na miji na Sh. 20,000 kwa ghorofa lote kwa maeneo ya vijijini.

Aidha, aliwakumbusha wafanyabiashara kutoa risiti za mashine ya kielektroniki (EFD) kwa kuwa inasaidia katika utunzaji wa kumbukumbu za biashara na vile vile kuwa uthibitisho wa mwenendo wa biashara.

"Napenda kuwasisitiza wafanyabiashara wenye mauzo yanayozidi Sh. milioni 14 kwa mwaka watumie mashine na kutofanya hivyo wanatenda makosa," alisema Kayombo.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara ambao tayari wanazo mashine za EFD kuzitumia mashine hizo ipasavyo, kwa kutoa risiti kwa kila mauzo na risiti hizo ziwe na kiwango sahihi kilicho husika katika muamala huo.

Vilevile aliwakumbusha wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa yoyote na wahakikishe kiwango kilichoorodheshwa kwenye risiti kiwe sawa na kiwango cha pesa alichotoa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live