Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yahimiza matumizi ya risiti za kielektroniki

Efd Machineee.jpeg TRA yahimiza matumizi ya risiti za kielektroniki

Wed, 13 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkoa wa kikodi wa Temeke umeanza kampeni ya kuhimiza matumizi ya risiti za kielektroniki kwa jamii ili kuondoa hasara zitokanazo na kutotumia risiti halali za kielektroniki.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini hapa, Meneja mkoa wa kikodi Temeke, Emmanuel Maro amesema lengo kuu la kampeni hiyo iliyopewa jina la 'Tuwajibike' ni kuwakumbusha wananchi kwamba matumizi ya risiti hizo ni suala la kila mtu.

Amesema mikoa mingine ya kikodi imeshafanya na leo ni zamu ya Temeke huku kampeni ikilenga makundi matatu.

"Kundi la kwanza ni wauzaji bidhaa na huduma mbalimbali kutoa risiti halali na sahihi pindi wanapouza na kundi la pili ni wanunuaji ambao nao wanawajibika kudai risiti halali kielektroniki," amesema Maro.

Amesema kundi la tatu ni jamii kwa ujumla ambapo ina wajibu wa kuripoti taarifa zozote za ukiukwaji zinazokwamisha utolewaji wa risiti halali za kielektroniki.

Aidha ameeleza baadhi ya faida za matumizi ya risiti akisema ni kuhakikisha mapato ya Serikali hayapotei na kutunza kumbukumbu pia.

"Faida ya tatu ni kwamba kwa kutumia kumbukumbu hizo, tunaweza kufanya makadirio. Huwezi kufanya makadirio kama huna kumbukumbu," ameongeza.

Amesema kampeni hiyo inafanyika kwa kuwatembelea wateja katika maeneo yao ya biashara ili kujua wanavyotumia mashine za risiti hizo na kutatua changamoto walizo nazo.

"Kwa siku ya leo tutakuwa maeneo ya Mbagala Rangi Tatu, Zakhiem na Chamazi na kesho tutakuwa Kigamboni na maeneo yake yote," amesema Maro.

Aidha amesema suala la matumizi ya mashine za EFD ni la kizalendo kwani linasaidia kusimamia na kukuza ulipaji wa mapato.

Pia amewataka wananchi kulichukulia suala hilo kwa mtazamo chanya na kuliwezesha taifa kukusanya kodi kwa halali.

Aidha amewataka wafanyabiashara kununua mashine za kutolea risiti kutoka kwa wazabuni walioidhinishwa na mamlaka hiyo ili kuepuka kununua mashine ambazo hazina ubora stahiki.

"Kama kuna matumizi ya taarifa feki tunaomba tupewe na sisi tutapeleka Matilda idara yetu ya uchunguzi na tukibaini tatizo tutachukua hatua Kali za kisheria," amesema Maro.

Pia amewataka wananchi kuhakiki taarifa zilizopo Kwenye risiti wanazopewa na uhalisia wa bidhaa walizonunua kwani wapo wauzaji wanaotoa risiti ambazo taarifa haziendani na huduma wanazotoa.

"Suala sio tu kudai risiti, bali kudai risiti halali ambayo taarifa zake zinaendana na huduma uliyopatiwa," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live