Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yahamasisha namna ya kuhakiki ubora wa bidhaa

Trapic Data TRA yahamasisha namna ya kuhakiki ubora wa bidhaa

Sat, 26 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) imetoa wito kwa wananchi kuendelea kupakua programu tumishi (application) maalumu iitwayo App ya Hakiki Stempu kuhakiki ubora wa bidhaa mbalimbali kabla ya kuzitumia ili kujiridhisha na ubora wake.

Wito huo umetolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kuhusu mkakati wa ushirikishaji wananchi katika kampeni za Hakiki Stempu na Kamata Wote, leo Ijumaa Februari 25, 2022, jijini  Dar es Salaam..

Amesema kuwa App ya Hakiki Stempu humwezesha mtumiaji wa bidhaa zozote kuhakiki bidhaa kabla ya kuzitumia ili kulinda afya na kuiwezesha Serikali kupata kodi halali, kutokana na ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa bidhaa husika kupitia mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki (Electonic Tax Stamp – ETS).

Kidata amesema programu hiyo mbali na kulinda afya pia inalenga kumlinda mzalishaji wa bidhaa kwa kuzitambua bidhaa bandia zisiingie sokoni na kudhoofisha bidhaa bora zinazozalishwa na wazalishaji waaminifu na kuwalinda wafanyabiashara waadilifu wanaotimiza wajibu wao wa kuzalisha bidhaa bora kwa kufuata sheria na kulipa kodi stahiki.

“Kwa kupitia App ya Hakiki Stempu, mtumiaji anaweza kujiridhisha na uhalali wa bidhaa kwa kupata taarifa kuwa bidhaa hiyo imezalishwa/imeingizwa nchini na nani, lini, wapi.”, amesema Kidata na kuongeza.

“Na kwa hatua hiyo  atakuwa na uhakika kuwa bidhaa hiyo itakuwa imepita katika mikonio ya vyombo vingine vya Serikali vya udhibiti wa ubora.”

Advertisement Kidata amesema kuwa mfumo wa ETS, unaiwezesha Serikali kukusanya kodi halali na kwa uhakika kutokana na taarifa zinazopatikana moja kwa moja kwani mfumo huo huchakata taarifa hizo na kuzisafirisha kwenda kwenye mifumo ya TRA, pasipo kuingiliwa na mtu.

 “TRA inaendelea kuhamasisha wananchi kupakua App ya Hakiki Stempu, ili kulinda afya zao lakini pia kuweza kupata taarifa endapo bidhaa imezalishwa/ imeingizwa na mzalishaji/muingizaji anayefahamika na vilevile imelipa kodi stahiki kwa maendeleo ya Taifa.”, amesema Kidata.

Akizungumzia mfumo huo wa ETS, Meneja wa mradi huo, Innocent Minja amesema kuwa stempu za za kodi za kielektroniki  ni alama inayobandikwa kwenye bidhaa kuonesha kwamba hiyo bidhaa imelipa kodi ama taarifa zake za kikodi zinafahamiki

Amesema kuwa stempu hizo hubandikwa katika bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi na ndani ya nchi na kwamba kwa bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi stempu hizo zinaweza kubandikwa hukohuko au hapa nchini.

Amezitaja bidhaa zinazohusika katika mfumo huo kuwa ni pamoja na bdihaa zote za vinywaji vikali na baridi, filamu na muziki na kwama wameanza na hizo kwa sababu zinalipiwa kodi ya ushuru wa bidhaa.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo amesema kuwa program hiyo inawezesha wananchi kuwasaidia watumishi wa TRA ambao hawawezi kuwepo kila mahali panapozalishwa au kuuzwa bdihaa, kushiriki uhakiki wa bidhaa hizo kwa faida ya afya zao.

Kuhusu kampeni ya Kamata Wote, Kidata alisema kuwa inalenga kuweka msukumo katika matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki za kodi (EFD) kwa muuzaji na mnunuzi.

“TRA inasisitiza wafanyabiashara kutoa risiti na wananchi kudai risiti kwa kila manunuzi au huduma wanazopata kwa lengo la kila Mtanzania kuchangia kodi.”, amesema Kidata.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz