Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA yaanzisha mfumo wa kielektroniki ritani za kodi

899401cf781e8d662f3b6a3e81b59330 TRA yaanzisha mfumo wa kielektroniki ritani za kodi

Sat, 8 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzisha mfumo wa uwasilishaji wa ritani za kodi kwa njia ya kielektroniki (e-Filing System) ukiwa na lengo kurahisisha uwasilishaji wa ritani za kodi na kupunguza gharama kwa upande wa mlipakodi.

Akizindua mfumo huo mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha juzi, Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Edwin Mhede alisema mfumo huo mpya utaongeza tija katika usimamizi wa kodi na kuboresha uwasilishaji wa ritani ambapo mlipakodi ataweza kuwasilisha ritani za kodi na kupata hati ya madai kwa ajili ya kufanya malipo bila kutembelea ofisi za TRA.

“Hii itapelekea kuondoa adha ya upotevu wa muda na rasilimali, kwa kuwa mfumo unamuwezesha mlipakodi kuwasilisha ritani za kodi wakati wowote hata siku za Jumamosi, Jumapili au Sikukuu,” alisema Dk Mhede.

Aidha, Kamishna Mkuu alieleza kuwa mfumo huu pia unamuwezesha mlipakodi kujua taarifa za ritani za kodi zinazotakiwa kuwasilishwa kwa kipindi husika na hivyo kuziwasilisha ndani ya muda stahiki na kuepuka faini ya kuchelewa kuwasilisha ritani hizo.

Alisema mfumo huu umetengenezwa katika namna ambayo unakumbusha mlipakodi tarehe ya mwisho ya kuwasilisha ritani na kulipa kodi zake stahiki na hivyo kupunguza uwezekano wa kutozwa riba na adhabu zinazotokana na kuchelewa kuwasilisha ritani na kulipa kodi stahiki kwa wakati.

Kamishna huyo alisema mfumo huo ni kiungo cha kurahisisha mawasiliano baina ya mlipakodi, Mkaguzi wa Mahesabu na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika majukumu ya kisheria ya kuidhinisha ritani za kodi pamoja na kuomba muda wa ziada wa uwasilishaji wa ritani endapo itabidi kufanya hivyo jambo ambalo litapunguza vitendo vya udanganyifu wa kughushi mihuri ya wakaguzi wa mahesabu katika kuidhinisha ritani za walipakodi.

Akizungumza kwa niaba ya washauri wa masuala ya kodi mwakilishi wa kampuni ya ushauri wa kodi ya PWC, Pamela Saleh alisema kuzinduliwa kwa mfumo huu utasaidia kupunguza misongo ya mawazo kwa wawasilishaji wa ritani za kodi kwa kuwa utawawezesha kuwasilisha kwa wakati.

“Mfumo huu wa uwasilishaji ritani za kodi utakuwa mfumo mzuri kwa kuwa utatuondolea stress, yaani msongo wa mawazo kwa kuwa tutawasilisha ritani za kodi wakati wowote na kutuepusha na fani za kuchelewa,” alisema Saleh.

Pamoja na mfumo wa sasa wa uwasilishaji wa ritani za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa njia ya kielektroniki, mfumo huu mpya (e-Filing System) utahusisha ritani zifuataz; Ritani ya Makadirio ya Kodi ya Mapato kwa watu binafsi; Ritani ya Makadirio ya Kodi ya Mapato kwa Taasisi; Ritani ya Kodi ya Mapato kwa watu binafsi; Ritani ya Kodi ya Mapato kwa Taasisi, Ritani ya tozo ya Mafunzo na Maendeleo ya Ufundi Stadi (Skills Development Levy - SDL) na Ritani ya Kodi ya Zuio katika mapato ya waajiriwa (PAYE).

Hata hivyo, wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya uchimbaji wa madini, mafuta na gesi wataendelea kuwasilisha ritani zao za kodi ya mapato kwa njia ya kawaida. Vilevile, ritani nyingine ambazo hazijatajwa hapo juu, zitaendelea kuwasilishwa kwa njia ya kawaida katika ofisi za TRA.

Mfumo huu wa uwasilishaji wa ritani za kodi kwa njia ya kielektroniki unaambatana na miongozo na mafunzo kwa walipakodi na wadau mbalimbali ili kujenga uwezo wa namna sahihi ya kutumia mfumo huu.

Mamlaka inawasihi walipakodi na wadau wengine kufuatilia kwa karibu miongozo itakayotolewa kwa njia mbalimbali za mawasiliano pamoja na kushiriki mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huu.

Chanzo: habarileo.co.tz