Mamlaka ya Ukusanyaji wa Mapato nchini (TRA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) zimetoa ufafanuzi wa baadhi ya maswali yaliyokuwa yakiwatatiza baadhi ya watu kuhusu utaratibu wa ulipiaji wa kodi ya majengo kupitia mita za umeme.
Akizungumza katika kipindi cha ‘Malumbano ya Hoja’ jana kinachoruka kupitia kituo cha luninga cha ITV, Kaimu Mkurugenzi Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi (TRA), Steven Kauzeni alisema utaratibu huo ni chini ya sheria ya usimamizi wa kodi namba 438 kifungu cha 56 ya Julai 2021. Katika kipindi hicho ambapo mada kuu ilikuwa “Utaratibu wa makato kodi ya majengo. Je unaeleweka kwa wadau wote?” maafisa kutoka Tanesco na TRA walijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wachangiaji.
Akijibu swali la mshiriki, Joel Msuya lililouliza ni kwa nini kuna nyumba moja ina mita zaidi ya moja na mita zote zinakatwa kodi na ikiwa ziko kwenye jengo moja? Kauzeni alisema mfumo wao unashindwa kutambua ni mita ngapi ziko katika nyumba moja hivyo mmiliki anapaswa kufika ofisini kwao ili ibaki mita moja ambayo ndiyo itakatwa kodi. Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma kwa Wateja Tanesco, Martin Mwambene alisema huwa wanakata kodi kwa kila mita kwa kutokujua na hivyo kusisitiza wamiliki kufika TRA na wao watafanyia kazi taarifa kutoka TRA. Kaimu Meneja wa Makusanyo yasiyo ya Kodi TRA, Joseph Amandus alisema Kuhusu suala la mpangaji kukatwa kodi badala ya mmiliki wa nyumba ni sheria ndio inawaelekeza kufanya hivyo pale wanapokosa namna ya kumpata mmiliki wa nyumba. Pia alipokuwa akijibu swali la Regan Mpogolo lililouliza kwanini mfumo huo ni baguzi kwa kulipisha kodi nyumba zenye umeme tu? Amandus alisema kodi hiyo inakatwa kwa majengo yote bila kujali kwamba jengo lina umeme au halina bali utaratibu huo ni katika kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi ambao nyumba zao zina umeme na kwa wale wasio na umeme wanapaswa kutumia utaratibu wa awali wa kwenda katika ofisi za mamlaka hiyo kulipia. “Kwa wamiliki wa majengo ambao wamefikia umri wa miaka 60 tunakuwa na utaratibu wa kuwasamehe kodi ya jengo, kwa hiyo mmiliki anapofikisha umri huo anaruhusiwa kufika ofisini kwetu na kututhibitishia na sisi tutamtoa katika ulipaji wa kodi,” alisema Amandus. Kauzeni pia alisema kwa wale waliokuwa wakielekeza tuhuma kwa TRA kwamba ni kwanini mamlaka hiyo iliwapelekea wamiliki wa nyumba mlundikano wa madeni, Kauzeni alisema wamiliki wa nyumba walipewa nafasi ya kwenda kulipia kodi walizokuwa wakidaiwa tangu 2021 lakini hawakufanya hivyo kwa kipindi cha miaka miwili na hiyo ndiyo sababu madeni yalikuwa makubwa. “Mfumo huu unawasaidia wamiliki wa majengo kutolimbikiza deni kwa kumfanya kulipa kidogo kidogo kwani kipindi cha nyuma walikuwa wakilalamika kushindwa kulipa kodi ya mwaka mzima kwa mara moja,” aliongeza Kauzeni.