Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

 TRA, Mamlaka ya Bandari zavunja rekodi mapato Januari

09359612f2138c94e47caef625b0f6fb TRA, Mamlaka ya Bandari zavunja rekodi mapato Januari

Mon, 14 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka za Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zimeendelea kuweka rekodi katika utendaji hasa ukusanyaji mapato katika kipindi cha Januari mwaka huu.

Hayo yalisemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Unguja, Zanzibar jana.

TPA

Kwa TPA kwa kipindi cha Januari pekee, imekusanya kiasi cha Sh bilioni 94.8 ikilinganishwa na Desemba mwaka jana ilipokusanya Sh bilioni 92.2, wakati TRA imekusanya Sh trilioni 1.7 sawa na asilimia 98 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 1.8.

Alisema kutokana na kasi ya utendaji wa mamlaka hizo, zimeendelea kuvunja rikodi kila mwezi.

“Na tafsiri yake ni moja, uwekezaji umefanyika na uboreshaji huduma umefanyika katika mamlaka ya TPA na matokeo yanaanza kuonekana,” alisema Msigwa.

Alisema kwa sasa meli 65 zinahudumiwa kwa mwezi katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo zamani zilikuwa zinahudumiwa meli 50 hadi 55 kwa mwezi.

Msigwa alisema pia bandari hiyo imeweka rekodi kwa Januari kuhudumia makontena 17,111 ikilinganishwa na makontena 13,575 yaliyohudumiwa Desemba, mwaka jana.

Alisema kwa mara ya kwanza bandari hiyo Januari 30 mwaka huu ilipokea na kuhudumia meli iliyokuwa na shehena ya madini ya shaba ya MV Papa John iliyokuwa na tani 41,000 ndani ya siku 10.

“Hii ni rekodi ya juu ambayo hatujawahi kufikia tani 41,000 ni nyingi na meli hii ni kubwa sana kuihudumia kwa siku 10 si jambo dogo. Hii inaonesha uwezekaji tulioweka katika Bandari ya Dar es Salaam unaleta manufaa makubwa,” alisema.

Msigwa alisema TPA imeendelea kuvunja rikodi ambapo mapato yameongezeka hadi kufikia Sh bilioni 94.8 kwa Januari ikilinganishwa na Desemba, mwaka jana ambako zilipatikana Sh bilioni 92.2.

Alisema katika maagizo yake ya kuboresha bandari nchini, Rais Samia Suluhu Hassan alitilia mkazo wa kutolewa Sh bilioni 210 kwa ajili ya kuboresha bandari nchini.

Alitaja baadhi ya mambo ya kuboreshwa yanayofanywa kuwa ni kununua mitambo takribani 20 ya kunyanyua mizigo yenye uzito wa tani tofauti kuanzia 42 ili kuhakikisha ushushaji wa mizigo unafanyika kwa haraka na ufanisi.

TRA

Kwa upande wa TRA, alisema makusanyo ya Desemba, mwaka jana ilivunja rikodi kwa kukusanya Sh trilioni 2.510 sawa na asilimia 107 ya lengo.

“Ukusanyaji mzuri wa mapato umeendelea kufanyika na ninayo furaha kuwaambia Januari, mwaka huu TRA imefanikiwa kukusanya mapato kwa asilimia 98, imebakisha asilimia mbili tu sawa na Sh trilioni 1.790,” alisema na kuongeza:

“Tupo vizuri katika ukusanyaji na mapato yetu hayajashuka na matarajio yetu wafanyabiashara wakiendelea kutambua kwamba kodi ni maendeleo tutakwenda vizuri na nchi yetu itapiga hatua katika maendeleo.”

Msigwa aliwataka wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla walipe kodi kadri inavyotakiwa kwani fedha zinazopatikana zinatumika kuboresha huduma mbalimbali ikiwamo miundombinu, afya, maji na elimu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live