Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imetoa mapendekezo tisa kwa Serikali ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na utendaji.
Mapendekezo hayo ni pamoja na kutaka ufanyike utekelezaji wa haraka wa mwongozo wa marekebisho ya kanuni za udhibiti ili kuboresha mazingira ya biashara (blueprint), kukamilisha sera ya kuendeleza sekta binafsi na kuongeza vivutio vya uwekezaji wa ndani na wa nje.
Zingine kupunguza urasimu, kuchochea uwekezaji kwenye sekta ya kilimo, upatikanaji mikopo na kuharakisha malipo ya madeni ya Serikali, kuongeza kasi ya ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya ubia (PPP).
Mapendekezo hayo yamewasilishwa kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki na Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte leo Jumatatu Februari 18, 2019.
Ziara ya Waziri Kairuki kwenye ofisi za taasisi hiyo ni ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo na Rais John Magufuli hivi karibuni.
Shamte amesema wameifanyia kazi Blueprint kwa miaka mitatu kutokana na kasi ya utekelezaji wake kuwa ndogo. "Kupitia kwako (Kairuki), tunaiomba serikali iharakishe utekelezaji wake" amesema Shamte.
Amefafanua kuwa sekta binafsi bado changa na sehemu kubwa siyo rasmi, walikubaliana kuchukua hatua za makusudi kuiimarisha, kuiendeleza na kuirasimisha ili iweze kuhimili ushindani wa ndani na nje lakini bado haijakamilika.
"Hili pia tunaomba lifanyike mapema ili tuitumie kurasimisha pia mifumo ya majadiliano kati ya sekta binafsi na umma katika ngazi zote ikiwamo vijiji, wilaya, mkoa, wizara na Taifa,” amesema Shamte.
Amesema Serikali iwawezeshe wawekezaji wa ndani na kuwe na makubaliano ya kisheria yanayoeleza kuwa kila uwekezaji kutoka nje unamshirikisha Mtanzania kumiliki hisa.
Amesema kuwe na juhudi za kuchochea kuhusu uwekezaji kwenye kilimo ili kutimiza lengo la kufikia Tanzania ya viwanda kwa sababu sekta hiyo ndiyo kubwa na hivyo inahitaji mapinduzi ya kilimo kiwe cha biashara na chenye tija.
Kuhusu miradi inayoweza kufanywa kwa ubia kufanywa na serikali Shamte alisema:
“Licha ya kuwapo kwa sera nzuri ya PPP inayosimamia miradi ya ubia lakini tunachokiona ni Serikali kuendeleza hamu ya kwenda yenyewe kwenye uwekezaji wa miradi ambayo ingeweza kufanywa kwa ubia.”
“Serikali ikifanya biashara na vyombo vyake yenyewe tu kama kinachoendelea kwenye ujenzi wa majengo ya serikali Dodoma ambapo miradi imepewa mashirika ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Suma JKT bila kushindanishwa kampuni za ujenzi za sekta binafsi" ameongeza
Akizungumza mara baada ya kupokea mapendekezo hayo Waziri Kairuki amesema jambo la kwanza atakalolifanyia kazi hatua kwa hatua, ofisi kwa ofisi ni suala la blueprint.
“Limekwama kwa muda, lakini sasa ninalifuatilia mwenyewe kuhakikisha linakamilika mapema iwezekanavyo,” amesema Kairuki.
Kairuki amefafanua suala la urasimu linafanyiwa kazi na kwa baadhi ya maeneo ni kama limekwisha na miongoni mwa vitu vinavyopigwa vita na kufanyika juhudi za kuvitokomeza ni urasimu.
Amesema pia atahakikisha wawekezaji wa ndani wanapewa kipaumbele kupata malighafi kabla hazijasafirishwa kwenda nje.
“Kwangu hii ni Wizara mpya, nasoma na kupitia vitu mbalimbali ili tufanye kazi vizuri na kwa pamoja, ninachowaomba ni ushirikiano wenu,” amesema
Kairuki amesema lengo ni kuwa na sekta binafsi yenye sauti, yenye nguvu na uamuzi.