Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPSF kuunganisha wadau kiuchumi, jamii

54ba79261f246eca4493e6261302582e TPSF kuunganisha wadau kiuchumi, jamii

Wed, 22 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imewahakikishia wanachama itaendelea kuwa kiungo muhimu kwa wadau ikiwemo sekta ya umma kufanikisha mageuzi ya uchumi na jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Dar es Salaam, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Angelina Ngalula mbali ya kuridhishwa na juhudi za taasisi hiyo, TPSF ipo imara na itaendelea kushirikiana na serikali katika kuwaletea Watanzania maendeleo ya kiuchumi.

Ngalula alisema taasisi hiyo itaendelea kutumia fursa zote ndani na nje ya nchi na kuwafanya wadau wazidi kunufaika kwa kutanua masoko la bidhaa zinazozalishwa na wadau wake na pia kuhamasisha na kukuza uwekezaji hapa nchini.

“Mkakati wetu sasa ni kutanua huduma zetu nje ya mipaka ya Tanzania na kuimarisha masoko ya ndani, ushiriki wa ujenzi wa miundombinu pamoja na kuendelea kufanya uwekezaji kwenye miundombinu iliyo tayari,’’ alisema.

Aidha aliwasihi wadau wa TPSF kuungana kipindi hiki ambacho imefanya mabadiliko ya uongozi baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Godfrey Simbeye kumaliza muda.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TPFS, Mbenna alisema atawaunganisha wadau wote na kuzidi kupanua majukumu ya taasisi kimataifa.

“Ni wakati wa kuwaleta pamoja wadau wa sekta binafsi na umma tuweze kusukuma maendeleo ya nchi yetu mbele zaidi,” alisema Mbenna.

Alisema lengo la taasisi hiyo ni kuwatumikia wadau wote nchini kwa kiwango cha juu cha utoaji wa huduma katika sekta zote za uchumi.

Mbenna alisema sekta binafsi itaendelea kuwa kiungo muhimu na kushirikiana na serikali kama mbia mkubwa na kutoa mchango katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Chanzo: habarileo.co.tz