Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPSF: Korosho zinaweza kununulika kwa bei elekezi

26652 Pic+tpsf TanzaniaWeb

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaa. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imesema kwa mujibu wa hesabu walizozifanya korosho inaweza kununulika kwa bei iliyoelekezwa na Serikali lakini faida ya wafanyabiashara itaathirika kwa kiasi fulani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 12, 2018, Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte amesema bei ya zao la korosho katika soko la kimataifa imeshuka kwa asilimia zaidi ya 40 ikilinganisha na msimu uliopita (2017/2018).

"Tunampongeza Rais John Magufuli kwa kusimamia kuhakikisha wakulima wanauza korosho kwa bei inayowapa faida.”

“Wanachama wetu wanasema inanunulika lakini faida inapungua sana kwa bei elekezi lakini sasa inapotokea jambo kama hili athari inabidi ziwe za pande mbili sio hasara kwa mkulima tu," amesema Shamte.

Amesema Tanzania haina uwezo wa kufanya jambo lolote unapotokea mtikisiko wa soko la dunia hivyo TPSF inashauri kuundwa kwa mfuko wa akiba wa mazao ili kusaidia wadau kuhimili hali zote hususani mabadiliko makubwa ya ghafla katika bei ya zao hilo.

Pia, taasisi hiyo imependekeza kutumia kituo cha Naliendele kufanya utafiti wa kujua gharama za uzalishaji wa zao hilo katika msimu husika ili iwe rahisi kupanga bei ya ukomo inayotoa faida kwa pande zote mbili.

Kadhalika TPSF imesema ni muhimu Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kuvifufua viwanda vya usindikaji na ubanguaji wa korosho au kuanzisha vipya na vya kisasa ili kuacha kuuza ghafi na badala yake shughuli zote zifanyike hapa kwa kuwa zao la korosho linaweza kuzalisha bidhaa nyingi mbali na chakula.



Chanzo: mwananchi.co.tz