Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limewaonya wananchi wa vitongoji vya Mamangwa na Kiloweko wilayani Mkuranga wanaofanya shughuli za kiuchumi eneo la mradi wa gesi asilia kwani kitendo hicho ni hatari na kinyume cha sheria.
Kauli hiyo imetolewa Machi 29.2023 Meneja Mawasiliano wa TPDC Marie Msellemu kupitia mkutano wa hadhara wa kuwapa elimu wanakijiji wa Mwanambaya kuhusu umuhimu wa wananchi kulinda miundombinu ya gesi.
Kupitia mkutano huo baadhi ya wananchi walieleza namna wanavyofanya shughuli za kiuchumi karibu na mradi wa gesi wakisema eneo lililopitiwa na mradi ni dogo hivyo sehemu iliyobaki wanatumia.
"Mradi umepita karibu na makazi yangu, kuna sehemu ya mita 60 karibu na mradi wa gesi hakuna katazo kwamba tusilime, kwahiyo mimi kwakuwa mradi umepitia karibu na makazi yangu hilo eneo pembezoni mwa mradi nalima mihogo na mazao mengine ya muda mfupi,"amesema Iddi Madenge mkazi wa Kijiji cha Mwanambaya.
Kufuatia kauli hiyo,Meneja Mawasiliano TPDC Marie Msellemu amesema kitendo cha wananchi kurudi kufanya shughuli zozote karibu na mradi wa gesi wakati tayari wamelipwa fidia ni kinyume cha sheria.
"Eneo la mita 60 kutoka kwenye mradi wa gesi hakuna shughuli yeyote inavyopaswa kufanyika, mtu atakayebainika kufanya hivyo atakaposhtakiwa hilo ni kosa la uhujumu uchumi, ni muhimu kutambua mradi huu unamanufaa makubwa,
Mtu unapolima athari yake ni kubwa kwasababu eneo la mradi halitakuwa imara hivyo inakuwa rahisi kwa uharibifu kutokea, pia unapolima karibu na eneo hilo ni hatari kwa maisha ya wananchi,"ameeleza.
Mbali na hayo, Marie amesema maeneo yote yaliyopitiwa na mradi wa gesi asilia wananchi wa eneo hilo husogezewa huduma muhimu za kijamii ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali pamoja na miradi mingine ikiwamo ya maji.
Amesema wilaya ya Mkuranga tayari Shirika hilo limefanya utafiti katika makazi ya watu na hivi karibuni nyumba zaidi ya 500 zitaunganishwa na gesi asilia wilayani hapo.
Naye Sultan Magembe mkazi wa Kijiji cha Mwanambaya ameliomba Shirika la TPDC kuwaunganishia nishati ya gesi asilia kwa matumizi ya majumbani kwani gesi ya mitungi inauzwa kwa gharama kubwa.
Mbali na gesi, amesema hawaruhusiwi kutumia mkaa kutokana na maeneo mengi kupata tishio la kuwa jangwa hivyo kwao gesi asilia ni nishati sahihi.
Naye Amina Mtanga mkazi wa Kiloweka ameiambia TPDC endapo watafanikiwa kuwaunganishia wananchi gesi asilia majumbani suala la ulinzi wa miundombinu hiyo litabaki kwa wananchi.
Kwa upanda wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanambaya Leila Chabuluma amesema wakishirikiana na vijiji jirani wanaendelea kuwaelimisha wananchi kupitia mikutano ya hadhara kuhusu umuhimu wa kutunza mradi wa gesi uliopita kwenye makazi yao.