Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPDC yasimamisha vigogo Tan Oil

Tpdc Picghn.png TPDC yasimamisha vigogo Tan Oil

Wed, 5 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), imewasimamisha kazi vigogo wa juu wa kampuni tanzu ya mafuta ya shirika hilo ya Tan Oil, wakidaiwa kufanya ubadhirifu katika uendeshaji wa taasisi hiyo.

Tan Oil inajihusisha na biashara ya uuzaji wa mafuta ya rejareja na ina vituo zaidi ya 10 katika mikoa mbalimbali nchini, kwa lengo la kuimarisha na kusogeza huduma za nishati kwa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa wizara hiyo, waliosimamishwa kazi jana ni Meneja Mkuu, Kapuulya Musomba, Meneja wa Fedha na Utawala, James Batamuzi, Meneja wa Hifadhi wa Mafuta, Sudi Abdallah na Meneja wa Usambazaji na Uendeshaji, Amour Marine.

Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta Musomba ambaye alisema: “sina comment’ (maoni) kwa sasa kama taarifa imesema hivyo, ndio hivyo…unataka niongee nini tena?” alihoji Kapuulya aliyewahi kuwa Kaimu Mkurugenzi mkuu wa TPDC.

Imeelezwa kuwa hatua hiyo, imefikiwa baada ya bodi ya wakurugenzi ya TPDC, kuelekeza kufanyika kwa ukaguzi wa kina wa uendeshaji wa kampuni ya Tan Oil, mchakato uliofanyika miezi michache iliyopita.

Ukaguzi huo, uliofanywa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali na kubainisha kuna viashiria vya ubadhirifu mkubwa katika uendeshaji wa taasisi hiyo.

Kutokana na hatua hiyo, Serikali kupitia bodi ya TPDC imeweka uongozi wa muda wa kuendesha shughuli za Tan Olil na kuiwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa Taasisi Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa hatua stahiki.

“Pamoja na hatua hii, bodi ya TPDC imeanza kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo ya kuongeza udhibiti na kuandaa mkakati mpya wa kibiashara wa Tan Oil,” ilisema taarifa hiyo.

Itakumbukwa kwamba takriban mwezi uliopita, Serikali ilibadilisha menejimenti ya TPDC katika jitihada za kuimarisha uendeshaji wa shirika, ikiwemo usimamizi wa kampuni tanzu za shirika hilo.

Alichosema waziri

Mwananchi lilimtafuta pia, Waziri wa Nishati, January Makamba kuzungumzia taarifa hiyo, ambaye naye alisema mbali na makosa hayo, watendaji hao pia walikuwa wakitoa taarifa za uongo wizarani na serikalini wakisema Tan Oil inafanya vizuri jambo ambalo si la kweli.

“Walikuwa wanatudanganya, ndio maana tukaamua kufanya ukaguzi wa kina kuhusu uendeshaji wao. Hatua za kusimamishwa kwao zimechukuliwa leo (jana), hatutavumulia mambo haya katika wizara hii “Hatutaishia katika Tan Oil tutafanya ukaguzi za utendaji na uendeshaji wa taasisi zote za wizara hii na kampuni zake tanzu, tukibaini ubadhirifu tunachukua hatua za haraka. Hii ni hatua ya kwanza tu,” alisema Makamba.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC, Balozi Ombeni Sefue alipoulizwa kuhusu undani wa suala hilo na muda wa kusimamishwa kwa viongozi hao, alisema: “hakuna muda maalumu.”

Sefue aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi aliongeza,”wamesimamishwa kupisha uchunguzi. Matokeo ya uchunguzi ndiyo yatawezesha Bodi kufanya maamuzi mengine. Kwa sasa hakuna hatua nyingine hadi Takukuru watakapokamilisha uchunguzi.”

Takukuru

Ili kujua kama majina ya vigogo hao yameifikia ofisi yake, Mwananchi lilimuuliza Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni kujua kama majina hayo yameshafika mezani kwake kwa ajili ya uchunguzi.

Alisema ni mapema kusema kama yamefika au hayafika katika chombo hicho cha kuzuia na kupambana na rushwa nchini. “Takukuru ni pana, nachelea kuthibitisha au kutothibitisha, kama majina yakifikisha kwetu, hii ni kazi yetu ya kila siku. Kwa sasa sina uhakika kama majina yamefika au la,” alisema Hamduni.

Chanzo: mwanachidigital