Dodoma. Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma(PIC) imeyataja mashirika matatu yanayojiendesha kwa hasara likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambalo limepata hasara ya Sh829.51 bilioni katika kipindi cha miaka mitatu.
Akisoma taarifa za kamati hiyo leo Jumamosi Februari 2, 2019 bungeni jijini Dodoma, mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Raphael Chegeni amesema mashirika mengine ni kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).
Amefafanua kuwa TPDC limekuwa likijiendesha kwa hasara kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2015 hadi 2016/17 na kwamba matumizi yamekuwa yakiongezeka ikilinganishwa na mapato yaliyokusanywa na kusababisha shirika kupata hasara.
Amefafanua kuwa mwaka 2014/15, TPDC ilipata hasara ya 297.71bilioni , mwaka 2015/16 hasara ya Sh374.62 bilioni na mwaka 2016/17 hasara ya Sh157.18bilioni
“Kupatikana kwa hasara ya muda mrefu kwa baadhi ya taasisi na mashirika ya umma kunachangia kwa kiasi kikubwa uendeshaji wa kusuasua kwa taasisi hizo kusababisha miradi mingi ya uwekezaji kushindwa kutekelezeka na kukamilika kwa wakati ili iweze kuleta tija iliyotarajiwa,” amesema.