Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPDC yajipanga kutoa gawio kwa Serikali

Fri, 15 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limejipanga kutoa gawio kwa Serikali mwaka 2019 baada ya mwenendo wake kuonyesha kupata faida katika kuendesha sekta hiyo.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Machi 15, 2019 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Kapuulya Musomba mbele ya kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ambayo imetembelea mitambo ya gesi ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

Musomba amesema shirika hilo limekuwa likijiendesha kwa hasara kwa muda mrefu lakini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wanafanya vizuri kwenye biashara.

"Kwa trend hii ya miaka mitatu iliyopita, ni wazi kwamba mwaka huu tutapata faida na kutoa gawio serikalini," amesema mkurugenzi huyo akiieleza kamati ya Bunge ya PIC,” amesema

Mkurugenzi huyo amesema shirika hilo lilianzisha kampuni tanzu mbili ambazo ni TanOil na Gasco ili kuongeza ufanisi wa shughuli za shirika hilo katika kusimamia rasilimali za gesi na mafuta kwa manufaa ya Taifa.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kamati ya Bunge, Raphael Chegeni amewapongeza TPDC kwa kuliondoa shirika hilo kutoka kuwa shirika mzigo kwa Serikali na kuwa shirika lenye faida linalotoa gawio kwa Serikali.

"Mmepiga hatua kubwa, siku zote kamati imekuwa ikiwanyooshea kidole kwa kutotengeneza faida. Mmefanyia kazi ushauri wa kamati na sasa mnatazamia kutoa gawio, hongereni sana," amesema Chegeni.

Mwenyekiti huyo amesema wanataka kuona Watanzania wananufaika na rasilimali yao ya gesi kwa kuona jinsi rasilimali hiyo inavyobadilisha maisha yao kupitia huduma mbalimbali za kijamii zinazotokana na mapato ya gesi.

Wabunge wametembelea miradi ya gesi ya Kinyerezi na Ubungo pamoja na mradi wa kusambaza gesi majumbani katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo Mikocheni, Mlalakua na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.



Chanzo: mwananchi.co.tz