Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPDC yaanika sababu kupanda bei ya dizeli

Mafuta Ya Petrol Kwa nini bei ya dizeli inazidi kupaa nchini

Fri, 4 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Licha ya Serikali kutia mkono katika uagizaji wa mafuta, bei ya dizeli bado haijatulia, hivyo kutishia ongezeko la gharama za uzalishaji na uendeshaji.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) juzi ilitangaza bei mpya ya mafuta na kwa yanayoingilia Bandari ya Dar es Salaam, lita moja ya petroli imeshuka kwa Sh21, huku mafuta ya taa nayo yakipungua Sh44 lakini dizeli ikipanda kwa Sh13.

Kwa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, bei ya petroli imepungua kwa Sh123 na dizeli kwa Sh92 kwa lita wakati ile ya Mtwara, Lindi na Ruvuma bei zikibaki kama ilivyokuwa mwezi uliopita.

Kwa sasa, bei ya petroli jijini Dar es Salaam ni Sh2,480 na dizeli Sh2,338, wakati Mtwara watanunua petroli kwa Sh2,534 na dizeli Sh2,425, huku Tanga wakilipia petroli Sh2,398 na dizeli Sh2,277. Wananchi wa Uvinza mkoani Kigoma watanunua lita ya petroli kwa Sh2,724 na dizeli Sh2,570.

“Mabadiliko haya yanachangiwa na mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji na thamani ya shilingi ukilinganisha na dola ya Marekani,” inasema taarifa ya Ewura.

Viwanda na malori yanayotumika zaidi kwenye usafirishaji wa mizigo ndio maeneo yanayotumia zaidi dizeli. Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Raheem Dosa alisema kupanda kwa bei ya dizeli jijini Dar es Salaam na mikoa inayoihudumia kunatokana na athari zilizopo katika soko la dunia ambako pipa moja linafika dola 90 sasa hivi.

“Serikali inachopaswa kufanya ni kutusaidia ni kupunguza kodi au tozo ili tuweze kuyapata kwa bei nafuu, hii itatusaidia kupunguza gharama za uendeshaji,” alisema.

Alisema mafuta yanachangia asilimia 70 kwenye gharama za uendeshaji katika sekta ya usafirishaji hivyo kuendelea kupanda kwa bei kutaathiri biashara, kwani ni ngumu kubadilisha bei kila siku.

Profesa wa uchumi, Delphin Rwegasira wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema ongezeko hilo la bei bado ni dogo na athari zake zinavumilika.

“Jambo muhimu ni kuchukua tahadhari, kwani mahitaji ya mafuta yanazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na dunia kuanza kupata nafuu ya mlipuko wa Uviko-19. Mabadiliko haya yamekuwa yakijirudia mara kwa mara hivyo ni muhimu kudhibiti bei,” alisema Profesa Rwegasira.

Katika jitihada za kukabiliana kupanda kwa bei, Oktoba 31 mwaka jana Serikali ililiruhusu Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuagiza mafuta kutoka kwa wazalishaji.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wauza Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya alisema hatua ya Serikali kuagiza mafuta haina athari yoyote.

“TPDC inapoingiza mafuta inakuwa kama wengine waliopo na utaratibu unabaki uleule na bei za duniani ni zilezile, mafuta yanayoingizwa na wao hayawezi kuleta unafuu tofauti na waagizaji wengine, ili kuleta unafuu labda Serikali iweke ruzuku,” alisema.

Mgaya alisema kwa kutumia meli zenye uwezo wa kubeba mzigo mkubwa ndipo gharama ya usafirishaji inaweza kupungua. Aliongeza kuingia kwa TPDC katika kuagiza mafuta kutaongeza upatikanaji wa nishati hiyo, hasa maeneo ya vijijini.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz