Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPDC sasa kununua mafuta kwa wazalishaji

Makamba Pic Data Waziri wa Nishati January Makamba

Sun, 31 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) limetangaza kuanza kununua shehena ya mafuta moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji jambo litakalowapa nafuu wanunuzi wa kati.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyikia jijini Arusha leo Jumapili Oktoba 31, 2021 Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kwa mara ya kwanza azma ya miaka mingi ya Serikali kununua shehena ya mafuta moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji imetimia.

"Hata kabla ya mwisho wa safari yetu mnamo Oktoba 28 mwaka huu tuliiwezesha TPDC kushiriki zabuni ya kiushindani na kampuni nyingine za kimataifa ambazo kila mwezi hushiriki zabuni kuleta mafuta nchini," amesema.

Makamba amesema TPDC imefanikiwa kushinda zabuni hiyo kwa kutoa bei ndogo zaidi ya kuagiza mafuta ya dizeli kwa Desemba mwaka huu ikiwa hali hiyo itapunguza makali ya bei ya mafuta na kudhihirisha kwamba hatua hiyo ina manufaa.

Makamba amesema Serikali imefanikiwa kushawishi nchi rafiki walizotembelea kushirikiana na Tanzania kujenga kituo kikubwa cha upokeaji na uhifadhi wa mafuta kwa ajili ya soko la ndani lakini kwa mahitaji ya nchi ya Afrika mashariki na kati na nyingine za mbali pale zinapohitajika.

"Kituo hiki kitatuhakikishia kuwa na kiasi cha kutosha cha mafuta ya ndani ya nchi wakati wote lakini kwa sasa iwapo itatokea dharura huko duniani na tukashindwa kuagiza mafuta kiasi yaliyopo nchini yanatutosheleza kiasi cha wastani wa siku 15 tu na kwa viwango vya kimataifa walau unapaswa kuwa na akiba ya siku 90," amesema.

"Baada ya wiki mbili kuanzia sasa kutakuwa na ziara ya viongozi na wataalam kutoka katika nchi tulizozitembelea kuja Tanzania kwa ajili ya kukamilisha taratibu za utekelezaji wa makubaliano hivyo wizara ya nishati itaendelea kuratibu na kufuatilia kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana kwenye ziara hiyo yanadumu na yanatekelezwa kwa maslahi mapana ya nchi ya Tanzania," amesema Makamba.

Chanzo: mwananchidigital