Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA yateka soko la bidhaa za Rwanda

Ad72d70902678a670e0dca1f1b487f01 TPA yateka soko la bidhaa za Rwanda

Tue, 14 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kutokana na mikakati endelevu ya kimasoko inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), soko la bidhaa za Rwanda limekua na kufikia takribani asilimia 90 kwa mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi, alibainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Meja Jenerali Charles Karamba.

Hamissi alisema kukua kwa soko hilo kumetokana na mikakati ya kimasoko inayofanywa na TPA nchini humo.

“Pamoja na mikakati yetu ya kimasoko, pia tunaishukuru jamii ya wafanyabiashara nchini Rwanda kwa kuzitangaza na kutumia bandari zetu za Dar es Salaam na Tanga kupitisha bidhaa zao,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, TPA imeweka nguvu kubwa katika kurudisha uhusiano mzuri zaidi baina yake na jamii ya wafanyabiashara wa Rwanda ili kuendelea kuhudumia soko hilo kwa ufanisi zaidi.

Alimwahidi Balozi Karamba na jamii ya wafanyabiashara nchini humo kwamba TPA itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza ili kurahisisha na kuboresha zaidi huduma zinazotolewa na bandari zetu kwa wafanyabiashara hao.

“Mheshimiwa Balozi, tunakuahidi kuwa tutaweka mazingira mazuri zaidi katika kutoa huduma kwa bandari zetu ili kuongeza ufanisi na kurahisisha zoezi la utoaji wa mizigo katika bandari zetu,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa TPA.

Balozi wa Rwanda nchini, Meja Jenerali Karamba alisema ubalozi hauna budi kuwa karibu na uongozi wa TPA ili iwe rahisi kutatua changamoto zinazojitokeza.

“Mizigo inayopita katika bandari za Dar es Salaam na Tanga imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na hii inatokana na huduma nzuri tunazopata bandarini pamoja na maboresho ya miundombinu yanayoendelea,” alisema Karamba.

Kwa mujibu wa balozi huyo, uchumi wa nchi zao umeendelea kukua na hivyo kuchochea ukuaji wa shehena ya mizigo inayopita katika bandari za Dar es Salaam na Tanga kwenda au kutoka Rwanda.

“Kumekuwa na ongezeko kubwa la shehena ya mizigo inayotoka na kuingia nchini Rwanda kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga hivyo tumeona sisi kama ubalozi ni muhimu kuwa karibu na uongozi wa TPA ili kuwa rahisi kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwa urahisi,” alisema.

Shehena ya Rwanda inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Tanga imekua kutoka tani 922,135 mwaka 2017/2018 hadi tani 1,293,531 mwaka 2020/2021.

Bidhaa zinazosafirishwa zaidi ni za vyakula, vifaa vya umeme, ujenzi, pembejeo za kilimo na magari.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live