Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA yatakiwa kutoa gawio la Sh1 trilioni mwaka 2020

89500 Gawiopic TPA yatakiwa kutoa gawio la Sh1 trilioni mwaka 2020

Sat, 21 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini, Isack Kamwelwe ameitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuongeza gawio kwa Serikali kutoka Sh480 bilioni la mwaka 2018/19 hadi Sh1 trilioni mwaka 2019/20.

Amesema jambo hilo lisipotimia atamfukuza kazi mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, Deusdedit Kakoko.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 21, 2019 katika uzinduzi wa bodi mpya ya mamlaka hiyo yenye wajumbe saba ikiongozwa na Profesa Ignas Rubaratuka aliyeteuliwa kwa mara ya pili.

Waziri Kamwelwe amesema haridhishwi na ukusanyaji wa kodi bandarini, kuitaka bodi hiyo kulifanyia kazi eneo hilo na kuhakikisha TPA inakusanya kodi na kuongeza gawio lake serikalini.

“Ikitokea leo Rais John Magufuli ananifukuza kazi kwa sababu ya TPA kushindwa kukusanya kodi vizuri, binafsi sitotetereka sana kwani nitaendelea kuwa mbunge, ila nyinyi ndio  mtaathirika zaidi,” amesema waziri huyo.

Uzinduzi wa bodi hiyo umefanyika katika ofisi za mamlaka hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam.

Wajumbe wengine wa bodi hiyo ni, Malata Paschal, Jabir Bakari, Masanja Kadogosa, Ephrem Kirenga, Renatus Mkinga, Jayne Nyimbo na Dephine Magere.

Akizungumzia bodi hiyo, Profesa Rubaratuka amemhakikishia Kamwelwe kuwa watafanya kazi kikamilifu.

“Bodi kwa kushirikiana na wafanyakazi na wadau wengine, itahakikisha lengo la kutoa gawio la Sh1 trilioni linafanikiwa,” amesema Profesa Rubaratuka.

Chanzo: mwananchi.co.tz