Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA yatakiwa kujitangaza kimataifa

573b51331a001c8dd798d04711d9c746 Eneo la bandari jijini DSM

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kujitangaza kimataifa ili kuzivutia kampuni kubwa za usafirishaji mizigo kutumia bandari za hapa nchini kupitishia mizigo yao.

Wito huo ulitolewa na Makamu Mwenyekiti wa PAC, Japhet Hasunga baada ya kumaliza kikao na uongozi wa TPA jana, ikiwa ni sehemu ya kamati hiyo kukagua shughuli za taasisi za umma.

Kamati hiyo ilitembelea Bandari ya Dar es Salaam na kushuhudia meli zikishusha mizigo.

Hasunga alisema kutokana na uwekezaji ambao Serikali ya Awamu ya Sita imefanya, kwa sasa bandari za hapa nchini zina uwezo mkubwa wa kuhudumia meli kubwa na hivyo kama TPA ikizitangaza itateka soko la Afrika Mashariki na Kati yote kwa kuwa hakuna nchi zenye bandari zenye ufanisi kama Tanzania.

“Bandari zetu nchini serikali inaendelea kuziboresha, mfano Bandari ya Dar es Salaam serikali imetumia Dola za Marekani milioni 421 kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali.”

Kwa sasa kuna meli kubwa zinatumia bandari hii, sasa tunataka uwapo mkakati wa kuitangaza bandari hii na nyingine za hapa nchini ili zitumike kuvutia zaidi kampuni za kimataifa kutumia bandari za hapa nchini hasa hii Dar es Salaam,” alisema.

Hasunga alisema kama TPA ikizitangaza bandari zitazidi kupata wateja kutoka nchi za Malawi, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi nyingine nyingi na kuipongeza kwa usimamizi mzuri wa huduma za bandari hasa kwa kupunguza siku za kutoa mizigo bandarini kutoka siku tisa hadi tatu.

Alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Erick Hamis kwa kuanza kuwachukulia hatua wafanyakazi wanaokiuka maadili ya kazi na misingi ya taaluma zao, huku akionesha imani kuwa jitihada hizo zitaondoa wafanyakazi wababaishaji wote na kuzidisha ufanisi wa kazi utakaowezesha kuongezeka kwa mapato ya serikali.

Katika kufanikisha ongezeko la mapato, Hasunga ametaka kuharakishwa kwa uunganishwaji wa kipande cha Reli ya Kisasa (SGR) kwa ajili ya kubeba mizigo kutoka bandarini ili kuunganishwa na reli kuu kisha kusafirisha kwenda sehemu mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Pia amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuweka kituo kidogo cha kupozea umeme katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuhakikisha ufanisi wa utoaji wa huduma hasa uboreshwaji wa miundombinu utakapokamilika na kuanza kutumika.

“Nawapongeza TPA kwa kuendeleza ufanisi na hasa suala zima la kupitia upya mikataba mbalimbali ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na uhalali wa mikataba hiyo, hivyo ninataka zaidi kuongezeka kwa utatuzi wa kero mbalimbali ili kuendana na kasi ya sasa ya ukusanyaji mapato,” alisema Hasunga.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Hamis aliihakikishia kamati hiyo kuwa kwa kushirikiana na wafanyakazi wote wa TPA ataendelea kuimarisha utendaji kazi wa bandari nchini, huku akisisitiza kuwa TPA itaendelea kutatua changamoto zote zinazokwamisha utendaji kazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live