Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imepunguza tozo mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumika kwa lengo la kuvutia wateja zaidi katika kipindi hiki chenye ushindani mkubwa wa kibiashara.
Ofisa Mkuu wa Utafiti na Masokowa TPA, Esaya Masanja amesema hayo alipokuwa akiainisha maeneo ambayo tozo hizo zimepunguzwa katika mkutano wa wadau wa kukusanya maoni juu ya maombi ya mapitio ya tozo waliyowasilisha kwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), mkoani Dar es Salaam.
Masanja amesema hilo limefanyika kutokana na ushindani uliopo katika Bandari ya Dar es Salaam na Mombasa, ambazo zote kwa pamoja zinafanya biashara kwa masoko wanayoyahudumia kwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Burundi na Uganda.
Amesema hayo yote yanafanyika ikiwa ni takwa la wadau kwa muda mrefu, hivyo aliainisha maeneo waliyopunguza tozo hizo ambazo marekebisho yake yalifanyika mwaka 2013 kuwa ni eneo la simu ambalo awali walitoza tozo kwa kutumia simu za mezani, lakini sasa teknolojia ya simu iko juu.
“Tozo inayotumika ya mwaka 2013 ni miaka 10 sasa na mambo mengi yamebadilika.
“Pia tumefanya marekebisho katika nchi za Malawi na Zambia ambako kuna tozo fulani walikuwa wakiitoa ambayo mteja akipitisha mzigo ilimlazimu kuitoa,” amesema.
Ameeleza mategemeo yao ni kwamba maboresho hayo ya tozo yataongeza wateja kutokana na mapunguzo hayo, pia TPA itakuwa kwenye nafasi nzuri katika soko la ushindani kwa kuwa watakuwa wameendana na mabadiliko ya biashara.
Amesema mategemeo mengine ni kuongezeka kwa mizigo kwa kuwa mwaka jana walihudumia tani milioni 18 katika bandari ya Dar es Salaam hivyo mategemeo ni kwamba mzigo utaongezeka.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Mkeyenge amesema shirika hilo lilipokea kutoka kwa TPA maombi ya mapitio ya tozo za bandari zinazoendeshwa na TPA katika bahari na maziwa.
Amesema maombi yaliyolenga kuhuisha tozo ili kuendana na mazingira ya biashara katika bandari za bahari na maziwa.
“Shirika limefanya tathmini ya awali ya maombi yaliyowasilishwa na kubaini kuwa yamekidhi matakwa ya kanuni za tozo na hivyo wadau wanaweza kutoa maoni yao,” amesema.
Amesema mkutano huo ni sehemu muhimu katika mchakato mzima wa uridhiaji wa maombi yaliyowasilishwa kwa kuwa unatoa fursa kwa watumiaji wa huduma za bandari na mtoa huduma, TPA kutoa maoni hayo kwa uwazi.