Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA yaona fursa lukuki Uganda

672063d40fb1fa131b0491c50c367bf2.png Bandari ya DSM imekua na utaratibu wa kujenga Ofisi nchi washirika

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi amesema TPA inaitazama Uganda kama fursa muhimu ya kiuchumi kwa Tanzania kupitia huduma za kibandari.

Hamissi ametoa taarifa hiyo katika ofisi mpya ya TPA nchini Uganda iliyopo Kampala iliyo katika hatua za mwisho kuanza kutoa huduma.

Kuanzishwa kwa ofisi hiyo kumelenga kuongeza ushawishi wa matumizi ya Bandari za Dar es Salaam na Mwanza kuhudumia shehena za nchi ya Uganda, malighafi za viwandani na kuwezesha bidhaa zinazozalishwa nchini humo zifike katika masoko.

Hamissi na maofisa waandamizi wa TPA walishiriki katika ziara ya siku mbili ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uganda.

Katika siku ya pili ya ziara hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alitembelea makao makuu ya Kampuni ya Roofing Group inayoongoza kwa kuzalisha vifaa vya ujenzi nchini Uganda.

Rais Samia alieleza utayari wa Tanzania kushirikiana na taasisi za Uganda kukuza biashara baina ya nchi hizo na kuikaribisha Roofing Group iwekeze Tanzania.

Mwenyekiti Mtendaji wa Roofing Group, Dk Sikander Lalani aliishukuru Tanzania kwa kuwezesha biashara ya kampuni hiyo kufanyika kwa ufanisi kupitia huduma za bandari za Dar es Salaam na Mwanza; Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Roofing Group na kampuni za uchukuzi za Tanzania zilisaini makubaliano ya kibiashara (SLA) Februari mwaka huu.

Makubaliano yanatajwa kuongeza kiwango cha shehena za Uganda zinazopita Tanzania kutoka asilimia mbili ya sasa hadi kufikia wastani wa asilimia 30.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano TPA, Nicodemus Mushi alisema kuwapo kwa ofisi hiyo kutawezesha huduma za kibandari kupatikana kwa ukaribu zaidi nchini humo.

“Kuwapo kwa ofisi mpya mjini Kampala tunaongeza uwezo zaidi wa kuhudumia wateja wetu toka pale walipo nchini mwao na hivyo kurahisisha shughuli zote za kuhudumia shehena iwe inaingia au inatoka Uganda kupitia bandari zetu nchini Tanzania,” alisema Mushi.

Ufunguzi wa ofisi ya TPA Uganda kutaimarisha matumizi ya bandari za Tanzania kwa nchi jirani ambazo hazina bandari. Tayari TPA ina ofisi Kigali (Rwanda), Bujumbura (Burundi), Lubumbashi (DRC) na Lusaka (Zambia).

Uamuzi wa kufungua ofisi mjini Kampala ni matokeo ya ziara ya siku tatu ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda nchini Tanzania mwaka jana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live