Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA yajipanga kuingiza shilingi trilioni 1.2

9152be895bf09a8801cc64b351643917.jpeg TPA yajipanga kuingiza shilingi trilioni 1.2

Sun, 14 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika mwaka 2022/2023 imepanga kukusanya takribani Sh trilioni 1.224 wakati Sh bilioni 762.606 zikipangwa kutumika kwenye miradi ya uwekezaji ikiwemo vitendea kazi.

Kati ya fedha za miradi ya uwekezaji, Sh bilioni 662.49 ni mapato ya ndani na Sh bilioni 100.112 ni kutoka Serikali Kuu ikiwa ni ruzuku kwa utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa jijini hapa na Mkurugenzi wa Mipango, Ubora na Udhibiti wa Vihatarishi, Dk Boniphace Nobeji wakati akizungumzia utekelezaji wa shughuli za Mamlaka na mwelekeo katika mwaka 2022/2023 alioutoa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu.

Alisema bajeti hiyo imelenga kutekeleza shughuli mbalimbali za TPA ikiwemo shughuli za uendeshaji, ununuzi wa mitambo, uboreshaji wa miondombinu ya bandari za bahari kuu na maziwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za kibandari na kuongeza ushindani wa Bandari za Tanzania na kutangaza bandari za Tanzania ndani na nje ya nchi.

Aidha, Dk Nobeji alisema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 TPA ilikusanya Sh trilioni 1.095 sawa na asilimia 97.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 20.3 ya mapato ya Sh bilioni 910.4 yaliyokusanywa mwaka 2020/2021. Akizungumzia utendaji kazi wa TPA katika kipindi cha kati ya Julai 2021 hadi Juni 2020, Dk Nobeji alisema shehena iliyohudumiwa ni tani milioni 20.665 sawa na ongezeko la asilimia 16 ya tani milioni 17.775 milioni zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2020/21.

Alisema pia idadi ya makasha ilifikia 823,404 sawa na ongezeko la asilimia 12 ya makasha 735,442 yaliyohudumiwa katika kipindi kama hiki mwaka 2020/22. Kuhusu shehena ya magari, Dk Nobeji alisema ni 203,932 sawa na ongezeko la asilimia 38 ya magari 147,566 yaliyohudumiwa mwaka kwa mwaka 2020/2021 wakati shehena ya masoko ya nchi jirani ilikuwa tani milioni 7.801 sawa na ongezeko la asilimia 39.9 ya tani milioni 5,580 iliyohudumiwa mwaka2020/21.

Nchi jirani zinazohudumiwa na Bandari ya Dar es salaam ni Jamhuri ya Kiemokrasia ya Congo(DRC), Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi, Uganda, Zimbabwe, Comoro na Sudan Kusini. Akizungumzia mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika sekta ya bandari, Dk Nobeji alisema Bandari ya Dar es Salaam ilipokea na kuhudumia meli kubwa ya MV. GLAND DUKE PANAMA iliyoshusha magari yapatayo 4,041 ikiwa ni idadi ya juu ya magari kuwahi kuhudumiwa katika Bandari za Tanzania.

Pia Bandari ya Dar es Salaam ilipokea na kuhudumia meli ya Shaba MV PAPA JOHN ambayo ilipakia tani 41,000 ya mizigo huku Bandari ya Tanga ikiweza kuhudumia meli kubwa za mafuta kwa kushusha jumla ya tani 114,707 kwa meli tatu na kuvunja rekodi ya bandari hiyo.

Alisema Bandari ya Tanga pia imehudumia meli ya clinker ya Mv. Star Fighter iliyobeba tani 49,500 ikiwa shehena kubwa kwenda Rwanda kuwahi kuhudumiwa katika bandari hiyo. “Aidha, Bandari ya Tanga imeweza kupakia kiasi cha tani za mafuta 8,559 kiasi kikubwa zaidi tangu Bandari ya Tanga ianze kuhudumia mafuta kupekeleka Zanzibar ukilinganisha na tani za mafuta 1,783 zilizowahi kuhudumiwa kwenda Zanzibar,” alisema.

Alisema kwa upande wa Bandari ya Mtwara ilipokea na kuhudumia meli ya MV Apria iliyokuja kubeba tani 32,444.84 za makaa ya mawe kwenda India, Meli ya MV. Star Fighter iliyokuja kubeba tani 59,500, meli ya MV. Kiran Marmara iliyokuja kubeba tani 59,815 kwenda India na Meli MV. ETG Southern Cross ambayo ndiyo iliyopakia mzigo mkubwa zaidi wa makaa ya mawe kiasi cha tani 59,960 kwenda Uholanzi.

“Kiasi hiki hakijawahi kuhudumiwa katika bandari ya Mtwara na hivyo kuifanya bandari ya Mtwara kufikia malengo yake na kuwa bandari endelevu isiyo tegemea msimu wa korosho pekee,” alisema. Dk Nobeji alisema Bandari ya Mwanza imeanza kuhudumia shehena ya makaa ya mawe kwenda Uganda na hadi kufikia Julai, 2022, tani 4,514 za shehena yamMakaa ya mawe zimesafirishwa kwenda Uganda.

“Aidha, tumeshuhudia ongezeko la shehena ya ngano kwenda Uganda na hadi sasa zimeshasafirishwa tani 4,000 za ngano… mafanikio haya yanatokana na juhudi za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuvutia wawekezaji nchini zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Dk nabeji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live