Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA yafungua ofisi Zimbambwe, Mbarawa aahidi neema

Mbarawa Tpa Tpa.png TPA yafungua ofisi Zimbambwe, Mbarawa aahidi neema

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali za Tanzania na Zimbabwe zimekubaliana kutafuta ufumbuzi wa kero zinazokwamisha kasi ya ukuaji wa biashara katika ushoroba wa Dar es Salaam.

Ufumbuzi huo ni pamoja na mamlaka ya bandari ya Tanzania (TPA), kutekeleza miradi mipya ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga gati mbili namba 12 hadi 15 na kutumia eneo lililokuwa likimilikiwa na Mamlaka ya EPZA kwa kujenga yadi kubwa ya kuhifadhia magari.

Hayo yamejiri leo Jumatatu Oktoba 16, 2023, kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa Ofisi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika jiji la Harare nchini Zimbabwe itakayokuwa na jukumu la kuiweka bandari hiyo karibu zaidi na wateja wake na kurahisisha ufanisi wa biashara kati ya mataifa hayo.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa ofisi hiyo, Waziri wa Uchukuzi,Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali ya Tanzania kupitia TPA, imejipanga kuongeza mchango wa Sekta ya Bandari katika Pato la Taifa kwa kuyafikia masoko yaliyopo katika nchi jirani.

“Tunataka kutoa huduma za viwango vya juu vya ubora ili kuhimili ushindani na kuzifanya bandari za Tanzania kuwa chaguo sahihi kwa wasafirishaji katika ukanda wa kusini mwa Afrika,”amesema

Awali, akitoa hotuba kwani niaba ya Serikali ya Zimbabwe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi na Miundombinu,Joy Makumbe amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara kati ya mataifa hayo hususan usafirishaji magari kupitia bandari ya Dar es Salaam.

“Hali hiyo inafanya Serikali ya Zimbabwe kuchukua hatua za makusudi za kusimamia ustawi wa biashara hiyo kwa kuondoa changamoto chache zilizopo,”amesema

Katika taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Juma Kijavara amesema, TPA inalitazama soko la Zimbabwe kwa umuhimu mkubwa na imejipanga kuelekeza nguvu zake katika kutafuta na kuzitumia fursa zilizopo.

“Tunaishukuru Serikali kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya bandari ambayo sasa inakua kwa kasi kutokana na ufanisi mkubwa wa huduma wa bandari zetu, ili kusafirisha shehena ya magari kuja Zambabwe,”amesema.

Amesema wanafanya maboresho makubwa katika miundombinu ya bandari kwa kunanunua vifaa vya kisasa na kufanya Kampeni za kimasoko za kitaifa na kimataifa kwa kushirikiana na wadau wote.

“Juhudi hizi zimeleta mapinduzi makubwa na matokeo yake ni ongezeko la shehena na mapato ya TPA, sababu inayotufanya kuelekeza nguvu zetu katika kuyafikia masoko ya nchi jirani ambazo tafiti zinaonesha kuwa, zipo fursa za kukuza zaidi wigo wa biashara yetu na mapato,”amesema.

Kijavara ameongeza kuwa ili kuongeza ufanisi zaidi, imekusudia kujenga maghala na miundombinu ya vyumba maalum vyenye majokofu ya kuhifadhia bidhaa zinazoharibika haraka (Cold Rooms)

Naye Balozi wa Tanzania Nchini Zimbabwe, Simon Sirro amesema, Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini Zimbabwe inaridhishwa na huduma za bandari ya Dar es Salaam kuitaka kufanya kazi kwa karibu na na Ofisi ya Ubalozi ili kuwezesha diplomasia ya uchumi kufanyika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live