Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA yaeleza sababu mkataba uwekezaji Bandari Dar kuwa siri

BANDARIII TPA yaeleza sababu mkataba uwekezaji Bandari Dar kuwa siri

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati baadhi ya wadau wakitaka kuwekwa wazi kwa mikataba ya uwekezaji na uendelezaji Bandari ya Dar es Salaam, Serikali imesema ni vigumu kutekeleza hilo, kwa kuwa ni kinyume na matakwa ya kisheria.

Mikataba hiyo ya miaka 30 ni ilisainiwa juzi Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Dubai kupitia Kampuni yake ya DP World.

Baada ya kusainiwa, baadhi ya wadau waliozungumza na Mwananchi, kwa nyakati tofauti walipongeza hatua hiyo na kutaka mikataba iwekwe wazi ili kuwapa fursa zaidi ya kuisoma na kuichambua kwa kina.

Miongoni mwa waliozungumzia jambo hilo ni Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Chama cha ACT-Wazalendo.

Katibu Mkuu TEC, Padri Charles Kitima aliyekuwepo Ikulu wakati mikataba hiyo ikisainiwa alisema maaskofu wanasubiri kuona maandishi ya kilichomo ndani.

“Maaskofu wanahitaji kuusoma, kusikia tu hakutoshi. Walikuwepo watatu kushuhudia tukio na walipoitwa hawakuambiwa kuna nini, lakini walichosikia wameona angalau kuna kusikilizwa kwa maoni ya wananchi na maaskofu walikuwa wanawasemea kwa sababu rasilimali za wananchi zilikuwa hatarini,” alisema

Mkurugenzi wa Jukata, Bob Wangwe alisema ili kujiridhisha na kauli kwamba mikataba hiyo imezingatia maoni ya wananchi ni vema ikawekwa wazi.

Kwa wao ACT Wazalendo walisisitiza hoja ya uwazi wa mikataba hiyo kwa jamii kwa kuwa Serikali inawajibika kwa wananchi wanaotakiwa kujua kilichomo.

Mikataba iliyosainiwa ni mkataba wa nchi mwenyeji (HGA), mkataba wa upangishaji ardhi na mkataba wa uendeshaji wa bandari gati 4 – 7 na uendeshaji wa pamoja wa gati 0 – 3 kati ya TPA na DP World kwa shughuli za kibiashara na za kiserikali.

Kauli ya TPA

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa alisema sheria za kimkataba zinazuia kuwekwa wazi kilichomo ndani.

Mbossa akizungumza kwa simu akiwa nchini Zambia kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan alisema mikataba ya kibiashara kwa mujibu wa sheria haiwekwi hadharani.

“Mkataba wa kibiashara kati ya TPA na DP World haitolewi hadharani kwa sababu kila mtu ana washindani wake,” alisema

Alisema kipo kifungu cha sheria kinachosisitiza usiri kwa pande zote na kuheshimu makubaliano na kikikiukwa kinaweza kusababisha kuvunjwa kwa mkataba na au fidia.

“Ukikiuka unaweza kusababisha kuvunja mkataba au kulipa fedha tena zinaweza kuwa nyingi tu. Lakini ukiwaonyesha washindani wake wanaweza kusema mbona hawa mmewapa mambo mazuri na ukiwaonyesha washindani wetu wanaweza kutumia vibaya. Lakini kama kuna mtu anataka kuiona kuna njia za kufuata,” alisema

Hata hivyo Mbossa hakueleza njia zinazopaswa kufuatwa kwa mtu anayetaka kujua kilichomo ndani ya mikataba hiyo.

Kauli kama hiyo ilitolewa pia na mmoja wa walioshiriki majadiliano ya mkataba huo ambaye hakutaka kutajwa jina lake akisema kisheria mikataba ya kibiashara haiwekwi hadharani.

“Jamani ile si ni mikataba ya kibiashara na kisheria inakuwa siri, sasa wanatakaje iwekwe wazi, tuvunje sheria?” alisema.

Mwananchi, pia lilizungumza na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Harold Sungusia ambaye alisema kuwekwa wazi kwa mkataba kunatokana na makubaliano.

Alisema mara nyingi mikataba ya kibiashara haiwekwi hadharani kutokana na vifungu vya usiri vinavyotaka watu wachache ndiyo waone kilichomo.

Hata hivyo, mwanasheria huyo alisema kuwekwa wazi kwa mkataba huo kutasaidia kuongeza uwajibikaji na kudhibiti rushwa pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kueleza maoni yao juu ya jambo hilo kwa kuwa lina masilahi ya taifa.

"Kwa miaka mingi, hata wabunge wamekuwa wakilia kunyimwa mikataba mingi ambayo Serikali imeingia na kampuni binafsi na hata wakiipata inaweza kuchelewa kujadiliwa na kufanya uamuzi juu ya suala hilo," alisema.

Kutokana na hilo, Sungusia alipendekeza mabadiliko ya kifungu cha sheria kinacholazimisha usiri ili kandarasi ambazo Serikali inatia saini ziwekwe wazi na kuongeza uwajibikaji.

Katika shughuli ya utiaji saini, Rais Samia alisema Serikali ilisikiliza michango na maoni mbalimbali iliyotolewa na TLS, vyama vya siasa, wanaharakati huru, vyombo vya habari, viongozi wa dini na wastaafu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live