Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA yaagizwa ikamilishe bandari kavu ya Kwala

3542b02b6c8b05d207b2d63eaf93bca7 TPA yaagizwa ikamilishe bandari kavu ya Kwala

Thu, 7 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inamaliza taratibu zote zinazohusika na ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ili iweze kuanza haraka hatua itakayoipunguzia mzigo Bandari ya Dar es Salaam.

Mwakibete alitoa maagizo hayo jana alipoitembelea bandari hiyo ambayo kwa sasa ujenzi wake umesimama licha ya kutajwa kwamba itakapokamilika itahudumia kontena 3,500 na kuipunguzia mzigo Bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa asilimia 60.

Ujenzi wa bandari hiyo umefikia asilimia 65 na mkandarasi anadaiwa kushindwa kwenda na wakati hivyo kusababisha mkataba kuvunjwa.

Sababu nyingine ni kucheleweshwa kwa malipo ya mkandarasi anayejenga barabara inayotoka Vigwaza hadi eneo la Kwala kwa kiwango cha lami, inayosimamiwa na Wakala wa Ujenzi wa Barabara nchini (TANROADS) ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 61. Mwakibete aliitaka TPA kumlipa mkandarasi anayejenga barabara hiyo.

Meneja Miliki wa Mradi huo kutoka TPA, Alex Ndibalema alisema taratibu zote za malipo ya mkandarasi huyo zimeshakamilika na wakati wowote kuanzia sasa atakabidhiwa.

"Kwa kuwa mmesema malipo kwa ajili ya mkandarasi anayejenga barabara yapo tayari, hakikisheni analipwa ndani ya wiki hii na mara moja aanze kazi ya kukamilisha ujenzi huo, lakini kuhusu ujenzi wa bandari pia hakikisheni mnakamilisha taratibu za cheti kwa ajili ya mkandarasi ili aweze kuanza kazi mara moja," alisema Mwakibete.

Alisema kukamilika mradi huo ni muhimu kwani kutasaidia Bandari ya Dar es Salaam kupunguza msongamano wa mizigo na hivyo kuiwezesha kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma. Ndibalema alisema Sh bilioni 84.2 zinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa mradi huo.

Alisema Sh bilioni 36.1 zimetengwa ili kukamilisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 15.5 kutoka Vigwaza hadi Kwala (eneo la mradi) huku zaidi ya Sh bilioni 37 zikitarajiwa kutumika kukamilisha ujenzi wa bandari hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live