Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ameielekeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inaanzisha bandari maalum kwa ajili ya mifugo kwenye maeneo kama vile Tanga, Pangani au katika maeneo ambayo itaona yanafaa.
Akizungumza wakati wa ziara yake alipotembelea bandari ya Lindi Kihenzile amesema, Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Afrika hivyo ni lazima kuwepo na bandari hiyo.
Amesema sio jambo jema kuchanganya mifugo na mizigo mingine kama vile mazao ya chakula, saruji na makaa ya mawe.
Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kuwa kwa kuzingatia juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya mifugo nchini, upo uhitaji wa kwenda na kasi hiyo kwani kwa sasa nchi jirani wana bandari kubwa maalum kwa ajili ya mifugo.
Aidha, ameielekeza TPA kukamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari nyingine mkoani Lindi katika eneo la Mitwele.
Naibu Waziri Kihenzile amekamilisha ziara yake ya siku mbili katika mikoa ya Mtwara na Lindi, iliyokuwa na lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni wakati wa ziara yake katika mikoa hiyo.