Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA sasa kuwachukua wafanyakazi wa Ticts

BANDARIII TPA sasa kuwachukua wafanyakazi wa Ticts

Fri, 9 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati mkataba wa Kampuni Binafsi ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (Ticts) ukielekea ukingoni, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepanga kuwachukua wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Hatua hiyo inakuja baada ya mkataba wa miaka mitano waliosainiwa Julai 6, 2017 kufikia ukomo Septemba 30, mwaka huu, licha ya kuwepo kipengele cha kuuhuisha lakini menejimenti ya TPA imekataa.

Ticts imehudumu Bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 22 sasa, tangu iliposaini kutoa huduma ya makontena na mizigo mingine, kazi ambayo itafanywa na TPA

Taarifa kutoka ndani ya mamlaka hiyo zinaeleza tayari mipango ya kuwachukua wafanyakazi hao inaendelea.

“Hatuna sababu ya kutafuta wafanyakazi wengine, wale wafanyakazi wa Ticts tunawabakisha, wako zaidi ya 600 na watakuwa wanalipwa vile vile. Hatutaki wapate shida na sisi tupate shida ya kutafuta wengine,” alisema mmoja wa maofisa wa juu ndani ya TPA ambaye hakutaka kuandikwa gazetini.

Alisema, kuanzia Januari 1 mwaka huu, Ticts haitakuwapo, licha ya kwamba inaendelea kuiomba menejmenti iendelee kutoa huduma lakini hilo limeshindikana kwa kuwa imeshindwa kufikia vigezo. Mwananchi ilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kujua undani wa mabadiliko hayo, ambaye alisema kwa sasa hawezi kulizungumzia suala hilo.

“Kama ni kweli ama uongo tusubiri. Tuwe na subiri,” alisema Mbossa. Alipoulizwa kama wameshindwa kukubaliana na Ticts, Mbossa alisema atafutwe wakati mwingine kwa kuwa hana majibu ya moja kwa moja.

Hata hivyo, gazeti hili lina taarifa za uhakika za kampuni hiyo kuandikiwa barua ya kuelezwa kusudio la kutokuongezwa mkataba, lakini jana Ofisa wa Ticts ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema bado hawajapokea taarifa rasmi kutoka TPA.

Alisema menejimenti ya Ticts imetaka yeyote asizungumze lolote na vyombo vya habari hadi hapo taarifa rasmi itakapotolewa.

“Tutakuwa na la kusema baada ya kupewa taarifa rasmi, kitakachofanyika tutatoa taarifa kuhusu hilo, kwa sasa hatuna cha kusema kwa kuwa hatujapokea taarifa kutoka TPA,” alisema.

Pamoja na kuwepo kwa hali hiyo, alisema wamekuwa wakikutana na TPA kwa ajili ya shughuli za kazi na si kwa majadiliano kwa kuwa yamefikia hatua inayohitaji kusubiri.

Kuhusu wafanyakazi, alisema ni ngumu kuzungumza hilo kwa kuwa haijaeleweka kama wamefikia mwisho kutoa huduma au la.

Mwezi uliopita, gazeti hili lilizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia Uchukuzi, Gabriel Migire kuhusu TPA kukusudia kuachana na Ticts, ambaye alisema kinachotakiwa ni huduma bora ndani ya bandari.

“Hadi TPA inafikia uamuzi huo nafikiri imechukua tahadhari hiyo na mtaendelea kuona,” alisema Migire alipoulizwa kuhusu TPA kuachana na kampuni hiyo.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara alipozungumza na gazeti hili mwishoni mwa mwezi uliopita juu ya kuondoka kwa Ticts na walivyojipanga alisema, mkataba rasmi wa kampuni hiyo unamalizika Desemba 31, mwaka huu.

“Kuanzia Januari mosi mwakani, Serikali kwa maana ya mamlaka ya bandari itachukua na huduma haziwezi kurudi nyuma hata kidogo.”

Akijibu swali aliloulizwa wamejipanga vipi kwenye eneo la vifaa ambavyo ni mali ya TICTS, Kijavara anayekaimu nafasi ya mkurugenzi mkuu alisema, “hilo halina shida kwa kuwa tayari tumekwisha leta ‘cren’ (mashine ya kunyanua vitu vizito) mbili.”

Kijavara alisema kuanzia Januari mosi mwakani watakapoanza kutoa huduma wao wenyewe, kitakuwa kipindi cha makabidhiano.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live