Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA inavyowezesha ushindani wa bandari Tanzania

849f93f19021197c9327cfb25a4d972d.jpeg TPA inavyowezesha ushindani wa bandari Tanzania

Fri, 17 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

“TUKO vizuri.” Anasema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi wakati akizungumza mafanikio ya Bandari ya Dar es Salaam huku akionesha vifaa mbalimbali na maboresho yaliyofanyika katika bandari hiyo ambayo ni kubwa na muhimu katika mfumo wa bandari nchini.

“Tuna mitambo ya aina mbalimbali ya kuhudumia shehena zinazoingia au kutoka katika bandari hii na bandari nyingine zote nchini. Pia tuna rasilimali watu wa kutosha wenye ubobezi mkubwa wa kuhudumia wateja na mizigo yao kwa saa 24, siku saba za wiki katika kasi kubwa lakini salama,” anasema Hamissi.

Mkurugenzi Mkuu huyo anasema kwamba kwa mabadiliko yanayotokea kwenye maeneo ya Kusini, Mashariki na Kati ya Afrika, bandari za Tanzania lazima zijiweke katika ushindani. Huku maeneo hayo yakiwa yamejijengea kanda zenye umuhimu mkubwa kibiashara, TPA imekuwa katika mpangilio wa kuweza kuhudumia wateja wake katika mazingira yenye ushindani. Kimsingi, kukua kwa biashara kati ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na dunia kunasababisha kuwepo kwa shughuli nyingi katika bandari kutokana na unafuu wa usafirishaji wa shehena kwa njia ya maji.

Inasemwa kwamba pale usafiri wa njia ya maji unapogharimu dola moja ya Marekani, Usafiri wa Reli utagharimu dola 5, wa barabara dola 7 na wa ndege dola 14, hivyo utaona usafiri wa maji ndio rahisi kuliko aina nyingine zote za usafiri. Kwakutambua yanayotokea katika biashara ya kimataifa na kikanda, TPA imekuwa katika harakati kubwa ya kuboresha na kujitangaza bandari zake kwa lengo la kuvutia wateja zaidi.

Hii ni pamoja na kufungua ofisi au mawakala katika nchi zinazotumia bandari zetu. Ikiwa na bandari tatu kubwa katika upande wa bahari na nyingine kadhaa katika maziwa, Tanzania imekuwa kiungo muhimu kwa nchi ambazo hazina bandari zilizopo Kusini mwa Afrika, Kati na Magharibi mwa dunia. Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara zimekuwa mlango muhimu kwa nchi za Malawi, Zimbabwe, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa Congo, Burundi, Rwanda na Uganda.

TPA ili kuleta karibu wateja imekuwa ikitekeleza mpango mkakati wake wa nne wa mauzo ya bandari kwa wateja kulingana na mahitaji ambao unatekelezwa kuanzia mwaka 2021-2026 kwa lengo la kuhakikisha kwamba bandari za Tanzania zinatumika kikamilifu.

“Bandari zetu zina mchango mkubwa kwenye uchumi wetu na chumi za majirani zetu ambao hawana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS), Matt Clift wakati alipokagua utendaji kazi kwenye Bandari ya Dar es Salaam Aprili 8, mwaka huu. Kulia ni Mkurugenzi wa Bandari Tanzania, Eric Hamissi. bandari,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano wa TPA, Nicodemus Mushi.

Anaongeza kwamba mauzo ya bandari yamelenga kuhakikisha kwamba inakuwa shindani huku ikiboresha biashara ya ndani na ya kimataifa. Anasema kwamba katika mkakati wa nne wa kuiuza bandari wanataka wananchi waelewe unafuu wa kutumia maji katika kusafirisha shehena kwani wanaweza kupunguza gharama hadi asilimia 40.

Katika juhudi za kuwaleta karibu wateja na kushawishi matumizi ya bandari za Tanzania, TPA imefungua ofisi katika nchi ambazo zinapitisha bidhaa katika bandari za Tanzania ikiwamo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Rwanda na Uganda. “Lengo la ufunguzi wa ofisi hizo ni kuhakikisha kwamba huduma za TPA zinatolewa kwa ufanisi mkubwa kwa kuwa karibu na wateja,” anasema Mushi.

Hali hiyo ya ufanisi inatokana na muundo ambao unawezesha diplomasia ya uchumi ambapo mameneja wa TPA katika nchi hizo wanashirikiana na balozi za Tanzania ili ndoto itimie. Wawakilishi hao kimfumo wanawasiliana moja kwa moja na Mkurugenzi Mkuu na hivyo kuhakikisha maamuzi yanachukuliwa kwa kasi na kwa usahihi.

Mushi anasema kwamba viongozi hao wanashughulika moja kwa moja na changamoto ya aina yoyote inayojitokeza katika kuhudumia mizigo ya wateja kutoka katika nchi husika. Umuhimu wao unatokana na ukweli kuwa wateja wengi wangelipenda kumaliza mambo yao wakiwa nchini mwao badala ya kusafiri hadi Bandari ya Dar es Salaam kupata huduma za masoko.

Ushindani kati ya Bandari ya Dar es Salaam na bandari za nchi jirani unazidi kuongezeka hivyo bandari inahitaji kujitangaza zaidi na kuwa karibu zaidi na wateja kutatua changamoto zao. Mushi anasema katika kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam na bandari zingine za Tanzania zinahimili ushindani na kuongeza shehena, Menejimenti ya TPA imetekeleza mikakati mingine zaidi ya kuanzisha ofisi ikiwamo maonesho ya Dubai Expo ambapo ilikutana na wadau na wasafirishaji shehena kupitia bandari za Tanzania na kuwashawishi kuanza kuendelea kutumia bandari za Tanzania.

Imefanya ziara za kimasoko katika miji ya Lubumbashi na Kolwezi nchini DRC na kukutana na wafanyabiashara mbalimbali kwa lengo la kuwashawishi kuendelea kutumia bandari za Tanzania hasa Bandari ya Dar es Salaam na kushiriki katika makongamano ya wafanyabiashara yaliyofanyika katika nchi za Uganda, Zambia na Rwanda.

Watendaji pia wamekutana na wafanyabiashara mbalimbali wa nje na kuwashawishi waendelee kutumia bandari za Tanzania kwa kuwa huduma zinaendelea kuboreshwa. Pia imeshiriki katika mikutano mbalimbali ya wadau wa bandari iliyofanyika katika mikoa ya Kigoma na Tanga na kukutana na wafanyabiashara na wadau wa Sekta ya Bandari kwa lengo la kujadili namna bora ya kuongeza ufanisi wa bandari zetu.

Jitihada zimeendelea kufanyika kuhakikisha bandari za Tanzania zinakuwa na matumizi endelevu ikiwamo TPA kupunguza tozo za kuhudumia shehena na meli kwa asilimia 30 kwa Bandari ya Mtwara na kuondoa gharama za kuhifadhi makasha tupu.

Ufunguzi wa ofisi katika nchi za nje zimesaidia kupunguza malalamiko ya wafanyabiashara ikiwamo suala la ucheleweshaji na huduma za kubabaisha kutoka kwa wakala wa usafirishaji bidhaa lililokuwa linalalamikiwa na wafanyabiashara wa Zambia. Waziri wa Uchukuzi na Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza kuhusu ufunguzi wa ofisi hizo alisema kwamba zinarahisisha mambo na pia kuweka uhusiano mzuri wa nchi kwa nchi.

“Jamii ya wafanyabiashara kwa ufunguzi wa ofisi hizo hawatakuwa na ulazima wa kusafiri kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kushughulikia shehena zao,” anasema Profesa Makame Mbarawa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live