Kigoma. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaboresha Bandari za Sibwesa na Lagosa zilizopo katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma kwa lengo la kurahisisha huduma za bandari kwa wananchi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali
Akizungumza jana Alhamisi Desemba 19, 2019 Meneja wa Bandari hizo, Percival Salama amesema ujenzi wa bandari hizo ni miongoni mwa miradi minne mikubwa inayotekelezwa na TPA katika mkoa wa Kigoma katika mpango wa mamlaka hiyo kuwa na bandari kubwa katika kila mkoa na wilaya inayopitiwa na maziwa.
Kwa upande wa bandari ya Sibwesa mradi uliogharimu Sh3.8 bilioni umekamilika kwa asilimia 100 ukihusisha ujenzi wa gati, jengo la abiria, ghala na vyoo.
Kwa sasa meli kubwa inatia nanga katika gati hilo lenye kina cha hadi mita tano hivyo kurahisisha usafirishaji wa mizigo mingi pamoja na abiria kwa wakati mmoja.
"Gati la Sibwesa lipo umbali wa saa tatu hadi nne kwa boti kufika nchi jirani ya DRC Mashariki katika jimbo la Karemi hivyo litarahisisha ufanyaji biashara na usafirishaji kati ya Tanzania na DRC pamoja na nchi za Burundi na Zambia," anasema Salama.
Anasema mazao yatakayosafirishwa kupitia bandari hiyo ni pamoja na mpunga, mazao ya uvuvi pamoja na mafuta ya mawese ambayo hulimwa kwa wingi mkoani Kigoma.
Mradi wa ujenzi wa bandari ya Lagosa, Salama amekamilika kwa asilimia 85 ikihusisha ujenzi wa gati, ofisi, jengo la abiria, ghala, vyoo na kibanda cha walinzi.
Meneja wa mradi wa Lagosa wenye thamani Sh12.5 bilioni, Pantaleo Mosha amesema mradi unaendelea vizuri na kwamba kazi kubwa iliyobaki ni kumalizia ujenzi wa gati litakalokuwa na urefu wa mita 180.
Mbali na miradi hiyo ambayo bado ipo katika hatua mbalimbali TPA, imeingia mkataba wa miaka miwili (kuanzia Septemba) na Kampuniya M/s XIAMEN ONGOING CONSTRUCTIONGROUP LTD kujenga bandari ya Karema iliyopo Wilayaya Tanganyika katika Mkoa wa Katavi.
Mradi huo una thamani ya Sh47 bilioni ambapo utahusisha ujenzi wa gati la mizigo na abiria, jengo la abiria, uchimbaji wakina na kizuizi cha mawimbi (breakwaters), majengo ya ofisi, maghala ya kuhifadhia mizigo na vifaa wezeshi katika huduma za kibandari.