MAKUBALIANO yaliyoingiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai (IGA) siyo mkataba kwa kuwa sifa mojawapo ya mkataba lazima uwe na malipo kama fidia ya huduma inayotolewa, hivyo kwenye IGA hakuna huduma yoyote inayotolewa kati ya nchi hizi mbili.
Kwa kuwa IGA siyo mkataba, hata kama isipotekelezwa hakuna upande utakaokuwa na nguvu kisheria ya kuushitaki upande mwingine kwa madai ya kushindwa kutumiza wajibu au majukumu waliyokubaliana.
Mwanasheria wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Kulwa Mumbuli anafafanua kuwa ili IGA ifanye kazi, lazima hatua ya kusaini mikataba ya uwekezaji baina ya serikari na mwekezaji (HGA) na ile ya utekelezaji kati ya mamlaka au taasisi husika na mwekezaji (Project Agreements). Mikataba hiyo ndiyo itakayoeleza haki na wajibu wa kila upande.
Mamlaka zilizopewa nguvu kisheria ya kuendesha na kusimamia mazungumzo ya kuingia mikataba ya utekelezaji ni TPA kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya DP World (DPW) kwa niaba ya Serikali ya Dubai.
Kupitia IGA, baadhi ya maeneo yatakayopewa kipaumbele cha ushirikiano ni uendelezaji na uendeshaji wa bandari ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam na si kuuza bandari hiyo au bandari nyingine yoyote.
Mumbuli anabainisha kuwa Ibara ya 5(1) ya IGA inaeleza wazi kuwa DPW atakuwa na haki ya pekee ya kuendeleza, kusimamia na kuendesha maeneo yote yaliyoorodheshwa katika Kiambatisho Na. 1.
Kwa mujibu wa Kiambatisho Na. 1 kinachoeleza maeneo ya ushirikiano, DPW itakuwa na wajibu wa kuendeleza, kusimamia na kuendesha Gati ‘0’ (RoRo), gati namba 1-4 yanayohudumia mizigo mchanganyiko na gati za makontena namba 5-7 katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Kwa hiyo majadiliano ya HGA na mikataba ya utekelezaji yatajikita katika maeneo haya. Hakuna sehemu yoyote kwenye makubaliano ya IGA inayosema DPW atachukua bandari zote za Tanzania. Serikali tumemweleza anaweza kuwekeza kwenye gati hizi zote, lakini kama DPW ataona anahitaji labda gati namba 1-4 tu, tutaingia naye mkataba kwenye gati hizo, gati zilizobaki tuna haki ya kumpa mwekezaji mwingine,” anasema Mumbuli.
Kuhusu baadhi ya watu kudai kuwa makubaliano hayo hayawezi kufanyiwa marekebisho na hayana ukomo, Mwanasheria huyo wa TPA anasema kuwa huo ni upotoshaji wa makusudi kwa kuwa Ibara ya 22 ya IGA inaeleza kuwa makubaliano hayo yanaweza kufanyiwa marekebisho wakati wowote pande hizo mbili zitakapokubaliana.
Pia anasema ukomo wa makubaliano hayo umeelezwa katika Ibara ya 23(1) ya IGA ambayo inabainisha kuwa makubaliano haya yatafikia ukomo ikiwa baadhi ya mambo yatatokea ikiwemo kuisha kwa shughuli za mradi, kufikia ukomo kwa HGA na mikataba mingine ya utekelezaji.
“Ibara ya 5(4) ya IGA inasema kuwa serikali zote mbili zimekubaliana kuhusu miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa katika awamu ya kwanza kama inavyoelezwa kwenye Kiambatisho Na. 1,” anaeleza Mumbuli.
Anaongeza: “Katika hili, Serikali ya Tanzania imejifunga kuwa haitaanzisha mazungumzo na mtu mwingine yeyote mpaka jambo moja au mawili yatokee ikiwemo kutokukubaliana kwenye majadiliano ya kimkataba au kama miezi 12 itaisha kabla ya majadiliano kukamilika,” anaeleza Mumbuli.
Migogoro
Kwa kuwa baadhi ya watu wanadai kuwa ni makosa kisheria kwa migogoro itakayotokea kwenye mikataba ya utekelezaji kusuluhishwa au kutolewa hukumu nchini Afrika Kusini, Mumbuli anasema kuwa nchi hizo mbili zilikubaliana kuwa migogoro yote itakayotokana na vipengele vya IGA itatatuliwa kwa mujibu wa Sheria za Uingereza kama inavyoelezwa kwenye Ibara ya 21.
Anasema kwa kuwa IGA inalinda uhusiano wa taifa na taifa, hivyo migogoro inayotokana na vipengele vya IGA haiwezi kutatuliwa na mahakama za taifa mojawapo kati ya mataifa hayo mawili yenye mgogoro ambayo ni pande za makubaliano ya IGA.
“Kwa hiyo mgogoro wa aina hii daima hutatuliwa na vyombo vya kisheria vya taifa jingine lisilofungamana na upande wowote wa mkataba husika (IGA). Hii ndio sababu ya migogoro itakayotokana na IGA kwenda kutatuliwa nchini Afrika ya Kusini,” anaeleza Mumbuli.
Mwanasheria huyo wa TPA anasema kuwa migogoro itakayotokana na mikataba ya HGA na mikataba ya utekelezaji ikiwemo mikataba ya utwaaji na utumiaji wa bandari itatatuliwa kwa Sheria za Tanzania.
IGA inaweza kuvunjika
Swali kama makubaliano yaliyoingiwa kati ya Tanzania na Dubai (IGA) yanaweza kuvunjwa au la, hilo linajibiwa kwenye Ibara ya 23 ya IGA.
Katika Ibara hiyo, Mumbuli anasema kuwa Ibara ya 23(1)(2)(3) zinasema kuwa makubaliano hayo yanaweza kuvunjwa baada ya pande zote kuwa kuridhia na ibara hiyo ndogo ya (1) inatoa ukomo wa makubaliano na mazingira yatayofanya makubaliano hayo ya IGA yafikie ukomo.
Pia anasema Ibara ndogo ya (2) inabainisha kuwa kama HGA itavunjwa kabla ya kufikia ukomo, IGA itaendelea kwa muda kwa lengo la kuruhusu upande utakaokuwa umeathirika kudai haki zake kama zitakuwepo na upande mwingine kutimiza wajibu wake utakao kuwepo.
Katika mazingira hayo, Mumbuli anasema kuwa, Ibara ndogo ya (4) inalinda haki za wahusika katika mikataba ya utekelezaji na kwa kuwa IGA ndio makubaliano mama, ikivunjika inasababisha migogo yote kufikia ukomo.
“Inawezekana serikali zikakosana kidiplomasia lakini TPA na DPW hawajakosana, hivyo ukiruhusu IGA ivunjwe moja kwa moja, maana yake TPA na DPW watalazimika kuvunja mikataba yao pia kwa sababu itakuwa haina miguu ya kusimamia, ndio maana Ibara ndogo ya (4) inalinda mikataba midogo kwa maana kwamba kama mikataba hiyo midogo haijapata dosari, basi IGA isivunjwe, kuahirshwa, wala kusitishwa katika mazingira yoyote,”anasema Mumbuli
Utaifishaji mali
Uwepo wa madai kuwa Tanzania haiwezi kutaifisha mali za mwekezaji, Mwanasheria wa TPA anasema kuwa hakuna popote kwenye Ibara ya 14(1) ya IGA inayosema kuwa Tanzania haina mamlaka ya kutaifisha mali za mwekezaji bali Tanzania inawahakikishia wawekezaji na wahusika wengine katika uwekezaji kuwa haina nia ya kutaifisha mali zao.
Anasema katika hali ya kawaida siyo rahisi nchi kuingia kwenye biashara huku kwenye mkataba unamwambia mwekezaji kuwa una nia ya kuja kutaifisha mali zake, na ndiyo maana serikali inawahakikishia kuwa haina nia ya kutaifisha mali zao.
Sheria mpya
Kutokana na hoja za baadhi ya watu kuwa makubaliano ya IGA yanaizuia Tanzania kutunga sheria mpya au kuingia mikataba mingine ya kimataifa, Mumbuli anasema huo ni upotoshaji.
Anasema Ibara ya 27 ya IGA inaeleza kuwa Tanzania haizuiwi kutunga sheria mpya yoyote bali inazuia pande za makubaliano kutotunga sheria au kuingia makubaliano au mikataba ya kitaifa na kimataifa itakayokinzana na utekelezaji wa makubaliano ya IGA pamoja na mikataba migine ya utekelezaji itakayotokana na makubaliano hayo.
“Kwa mfano unaingia mkataba na DPW ukimruhusu pamoja na mambo mengine aendeleze bandari kavu, baadae unasaini mkataba wa kimataifa unaopiga marufuku uendeshaji wa bandari za nchi kavu, maana yake tayari mkataba huo wa kimataifa utakuwa unakinzana na mkataba wako na DPW kwa kuwa utamfanya ashidwe kuendesha biashara yake,” anaeleza Mumbuli.
Anafafanua”Sheria au mikataba ya aina hii ndio inayozuiwa kutugwa au kuingiwa na wahusika wa IGA kitu ambacho ni sahihi kabisa. Hata katika biashara za kawaida, huwezi kumkodishia mtu gari kwa mwaka mzima ukiwa umeisajiri kama gari ya abiria, halafu miezi miwili au mitatu baada ya kumkodishia ukaenda kubadili usajiri wake kuwa gari ya mizigo.”
Mikataba
Kwa mujibu wa Ibara ya 28 ya IGA, kila upande wa makubaliano unalindwa na kutamka kuwa wanaosaini makubalianao hayo wamepata mamlaka kutoka serikalini chini ya sheria za nchi husika ambazo zinaelekeza namna ya kusaini mikataba ya kimataifa.
Kwa mantiki hiyo, Mumbuli anasema kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ilimteua Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kusaini kwa niba ya serikali na kwa Serikali ya Dubai ilimteua Mtendaji Mkuu wa Bandari na Forodha, Ahmed Mahboob Musabih kusaini kwa niaba ya serikali yake.