Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TIRDO wamshukuru Rais Samia kuwapa vifaa vipya vya maabara

TIRDO Wamshukuru Rais Samia Kuwapa Vifaa Vipya Vya Maabara.jpeg TIRDO wamshukuru Rais Samia kuwapa vifaa vipya vya maabara

Sun, 3 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) Prof. Mkumbukwa Madundo Mtambo amemshukuru Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha Shirika hilo kupata vifaa vipya vya maabara ambavyo vitarahisisha utendaji kazi wa shirika.

Prof. Mtambo amesema kuwa kwa sasa Sekta ya Viwanda inakua kwa kasi kubwa duniani kote kwa hivyo upatikanaji wa taarifa sahihi za kitaalam kupitia tafiti unahitaji. Sambamba na hilo, uwepo wa wataalam wabobezi na Maabara zenye vifaa vya kisasa ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za ukuaji wa uchumi kupitia viwanda.

Prof. Mtambo amezitaja Maabara zilizoweeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita hivi karibuni kuwa ni Maabara ya uchunguzi wa kikemia (Analytical Chemistry Laboratory) ambayo inatumika kwa utafiti na uchunguzi wa sampuli mbalimbali kubaini uchafuzi wa mazao na bidhaa za Kilimo kama vile sumu Kuvu (Mycotoxins), Maabara ya Teknolojia ya Chakula (Food Microbiology) ambayo inatumika kwa ajili ya utafiti na uchunguzi wa sampuli za Kibaiolojia, Maabara ya Ngozi na Nguo (Textile and Leather Testing Laboratory) ambayo hutumika kupima kwa utafiti na uchunguzi wa bidhaa za ngozi na nguo kabla na baada ya kuzalishwa.

Maabara nyingine ni maabara ya Nishati (Energy Laboratory) ambayo imepata vifaa vya kisasa kabisa yenye uwezo wa kupima ubora wa aina yoyote ya vifaa vya Nishati vikiwemo Makaa ya Mawe, Umeme, Briketi mbalimbali, nk; na Maabara ya Mazingira ambayo hutumika kwa Tafiti na uchunguzi ili kuwashauri na kuwasaidia wenye viwanda kuweza kupunguza uharibifu wa mazingira utokanao na uzalishaji viwandani.

Maabara zote hizi zimekamilika kwa asilimia mia moja na kwa sasa TIRDO ina uwezo mkubwa wa kufanya tafiti na kutoa huduma mbalimbali za kitaalam kupitia wataalam wake na maabara zake ili kusaidia maendeleo ya viwanda nchini. Maabara zilizowezeshwa zina uwezo wa kupima kila aina ya Sampuli inayofika kwa wakati na kwa usahihi zaidi," aliongeza Prof.Mtambo.

Prof. Mtambo anatumia nafasi kuwakaribisha wadau wote nchini kutumia Maabara za TIRDO hasa katika kipindi hiki ambapo Tanzania ni mwenyeji wa Mkutano wa Kilele cha mifumo ya Chakula Barani Afrika unaotarajia kuanza tarehe 5 hadi 8 Septemba,2023 jijini Dar Es Salaam (AGRF 2023). “Tukiwa na Bidhaa bora zizizohakikiwa na wataalam viwanda vyetu na wafanyabiashara wetu wataweza kutumia soko kubwa la Afrika”-aliongeza Prof. Mtambo.

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) ni shirika la utafiti na maendeleo ya Viwanda Tanzania lililoanzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 5 ya mwaka 1979 na lilianza kufanya shughuli zake tarehe 1 Aprili, 1979. TIRDO ni Shirika la Umma ambalo liko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara . Jukumu lake ni kusaidia sekta ya viwanda nchini kupitia utafiti na kutoa huduma za kitaalam kusaidia maendeleo ya viwanda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live