Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TIC yasajili miradi ya ajira 178,101

100b508dae1aa0aef91b23482d9d2abb TIC yasajili miradi ya ajira 178,101

Mon, 31 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 1,312 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 20.4 katika Kanda ya Kaskazini, itakayotoa fursa za ajira kwa Watanzania 178, 101.

Akizungumza katika semina ya wafanyabiashara na wajasiriamali wilayani Korogwe, Meneja wa TIC Kanda ya Kaskazini, Daudi Riganda, alisema uwekezaji huo umekwenda sambamba na utelezaji wa sera ya Tanzania ya viwanda.

"Kati ya miradi hiyo iliyosajiliwa, 365 ni ya wawekezaji wa ndani, 571 inatokana na uwekezaji wa kigeni, ambapo 376 inatokana na ubia kati ya wazawa na wageni," alisema Riganda.

Aliitaja sekta inayoongoza kwa idadi kubwa ya miradi kuwa ni uzalishaji viwandani ambayo imechukua takribani asilimia 54 ya miradi yote, huku kilimo ikiwa ni asilimia 39.

Aidha, Riganda alisema katika kipindi cha mwaka 2015 hadi Juni, 2020, miradi ya uwekezaji iliyoandikishwa na TIC kwa Kanda ya Kaskazini ilikuwa 192, huku mkoa wa Arusha ukiongoza.

"Mkoa wa Arusha tumeweza kusajili miradi 112, Tanga miradi 39, Kilimanjaro 24 na mkoa wa Manyara miradi 17, ambapo sekta za kilimo na utalii zikiongoza kwa kuwa na miradi mingi," alisema Riganda.

Meneja huyo wa TIC Kanda ya Kaskazini alisema mkoa wa Tanga pekee miradi iliyosajiliwa imeweza kuwekeza mtaji wa thamani ya dola za Marekani milioni 1.4 na inatarajiwa kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania 4.797.

Aliwataka wafanyabiashara na wajasiriamali kuitumia TIC kupata taarifa za fursa za kibiashara na uwekezaji zilizoko katika kanda hiyo ili kuinua uchumi na kujiletea maendeleo.

"Kitumie kituo hiki kwani kina fursa mbalimbali ikiwamo kupata misamaha ya kodi ya kuingiza bidhaa za mitaji kutoka nje kwa wajasiriamali waliosajiliwa na kituo hicho," alisema Riganda.

Kwa upande wao, wafanyabiashara waliiomba TIC kuwafikia wajasiriamali wengi na kutoa elimu kuhusu namna watakavyonufaika kutokana na shughuli zinazofanywa na kituo hicho.

"Hii elimu ndio mara ya kwanza kuipata kwa sisi wafanyabiashara na wajasiriamali, ingekuwa vema kama elimu hii ingewafikia hasa wazalishaji wa malighafi walioko katika ngazi za vijiji,” alisema, Waziri Athuman.

Michael Mwandezi alisema kilio kikubwa ni mitaji ambayo imekuwa kikwazo katika kuboresha na kukuza biashara na kuiomba TIC iwaunganishe na wawekezaji wa kigeni ili kuingia ubia.

Wakati huohuo, TIC imewaasa wajasiriamali wa chini na kati kujitokeza ili kunufaidika na huduma zinazotokewa na kituo hicho ili kuongeza uwekezaji wa ndani ya nchi.

Riganda alitoa wito huo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wafanyakazi na wajasiriamali wa wilaya ya Korogwe yenye lengo la kutambua fursa za kiuchumi zilizoko wilayani humo.

"Kumekuwa na dhana kwamba TIC imekuwa ikijali zaidi wawekezaji kutoka nje ya nchi jambo ambalo sio kweli, kwani hata Watanzania wanaweza kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo hapa nchini," alisema Riganda.

Awali, akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Kasongwa, aliwataka wafanyabiashara na wajasiriamali kuyatumia mafunzo hayo kuimarisha biashara zao.

Chanzo: habarileo.co.tz