Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TIC yasajili miradi ya Sh10 trilioni mwaka 2023

Pesa Fedhaddd TIC yasajili miradi ya Sh10 trilioni mwaka 2023

Tue, 9 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 504 yenye thamani ya Dola za Marekani 5.6 bilioni (takribani Sh10 trilioni) kati ya Januari hadi Desemba, 2023.

Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia zaidi ya 100 ikilinganishwa na miradi 132 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika kiwanda cha kuchakata na kusindika nyama cha Chobo Investments Company Limited eneo la Usagara Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza leo Januari 8, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema zaidi ya miradi 250 iliyosajiliwa kipindi hicho inamilikiwa na Watanzania.

Amesema zaidi ya fursa 100,000 za ajira zinatarajiwa kutengenezwa pindi miradi yote itakapokamilika.

“Serikali itaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kuvutia mitaji zaidi kutoka ndani na nje ya nchi; lengo kuu ni kusajili miradi mingi zaidi itakayoongeza siyo tu uzalishaji, bali pia kipato na fursa za ajira nchini,’’ amesema Teri

Kupitia mikakati hiyo, mtendaji mkuu huyo wa TIC amesema Serikali imepanga kuongeza idadi ya miradi inayomilikiwa na Watanzania kufikia miradi 1,000 mwaka 2024 kulinganisha na zaidi ya miradi 250 iliyosajiliwa mwaka 2023.

Ametaja kushusha kiwango cha mtaji wa kusajili mradi TIC kutoka Dola za Marekani 100,000 (Sh240 milioni) hadi Dola za Marekani 50,000, takribani Sh125 milioni.

‘’Serikali pia inatoa punguzo la asilimia 75 kwa ushuru wa forodha kwa wawekezaji wanaosajili miradi yao TIC wanapoagiza bidhaa za mtaji,’’ amesema Teri

Kupata huduma ya pamoja kutoka taasisi 12 za Serikali zikiwamo Baraza la Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), ni faida nyingine kwa wawekezaji wanaosaji miradi yao TIC.

Mkurugenzi wa Chobo Investments Company Limited, John Chobo ametaja ubora hafifu wa mifugo kutoka kwa wafugaji kutokana na lishe duni, kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya uchakataji na usindikaji wa nyama nchini.

‘’Tumelazimika kuanzisha shamba la mifugo kuwezesha kiwanda chetu kujitosheleza kwa mahitaji ya malighafi,’’ amesema Chobo

Katibu Tawala Msaidizi, Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Mwanza, Patrick Kalangwa amesema mkoa huo unaendelea kuweka mikakati itakayowavutia wawekezaji zaidi katika sekta ya ufugaji, uvuvi na kilimo kutokana na fursa zilizopo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema uongozi wa mkoa huo umepanga kuitisha vikao vya wadau wa uwekezaji kwa lengo la kueleza na kutangaza fursa

Chanzo: www.tanzaniaweb.live