Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TIC yasaini utekelezaji miradi 4 itakayotoa ajira 28,710

016eb0128838d39eaf12d8e4c43fc27f Kituo cha Uwekezaji nchini TIC

Sat, 26 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesaini mikataba ya utekelezaji miradi na kampuni zilizowekeza kwenye miradi ya kimkakati na mahiri ambayo uwekezaji wake una thamani ya dola za Marekani bilioni 1.1 na ukitarajia kutoa ajira 28,710.

Hafla ya utiaji saini ilihusisha kampuni nne kati ya sita ambazo zimepitishwa na Kamati ya Taifa ya Uwekezaji (NISC) baada ya kuridhishwa na kufikia vigezo vilivyoainishwa na kamati hiyo.

Akizungumza kabla ya utiliaji saini mikataba hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dk Maduhu Kazi alisema miradi hiyo ni muhimu na itakuwa na manufaa kwa nchi.

Alisema mradi wa kwanza ni wa Itracom wa kiwanda cha kuzalisha mbolea kitakachogharimu dola za Marekani milioni 180 huku kikitarajia kutoa ajira 4,500 za moja kwa moja na 6,000 ambazo si za moja kwa moja na kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 600,000 za mbolea kwa mwaka.

Dk Kazi alisema pia Mradi wa Bagamoyo Sugar wa kilimo cha miwa na kiwanda kwa ajili ya uzalishaji wa sukari utakaogharimu dola za Marekani milioni 193.75 na kutoa ajira 1,500 za moja kwa moja na 10,000 ambazo si za moja kwa moja. Kitazalisha tani 300,000 za sukari na hivyo kupunguza mahitaji ya uagizwaji sukari kutoka nje.

Alisema mradi mwingine ni wa Taifa Gas wa kuchakata gesi utakaogharimu dola za Marekani milioni 62 na kuleta ajira 60 za moja kwa moja.

Dk Kazi alisema pia mradi wa Kagera Sugar wa kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari utakaogharimu dola za Marekani milioni 410, kutoa ajira 10,000 za moja kwa moja na 50,000 ambazo si za moja kwa moja, na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za sukari.

Alisema pia Mradi wa Mtibwa Sugar ambao ni wa kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari, utakaogharimu dola za Marekani milioni 150, na kuwa na jumla ya uwekezaji wa dola za Marekani milioni 305 na kuleta ajira 12,500.

Dk Kazi alisema mradi mwingine ni Knauf unaotekelezwa na mwekezaji kutoka Ujerumani ambao ni wa kuzalisha bodi ya dari na jasi na utagharimu dola za Marekani milioni 105, ukitoa ajira 150 za moja kwa moja na 500 zisizo za moja kwa moja, na kikiwa na uwezo wa kuzalisha mita za mraba milioni minne kwa mwaka.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiliaji saini huo, Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema serikali imeendelea kuondoa ukiritimba ili kuwavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live