Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TIC yamnyooshea kidole DC aliyemkadiria kodi mwekezaji

14243 Tic+pic TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimewataka viongozi wa Serikali kuacha kutoa maagizo na kujichukulia hatua bila kuwasiliana na mamlaka husika katika uwekezaji.

Kauli ya TIC imekuja siku chache baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya kuagiza kukamatwa kwa mkurugenzi wa kampuni ya Tudeley Estates Ltd inayomiliki mashamba kwa madai ya kukwepa kodi ya Sh713 milioni kwa miaka saba.

Ole Sabaya aliiamuru Idara ya Uhamiaji wilayani Hai kumnyang’anya hati ya kusafiria meneja wa kampuni hiyo, Trevor Gifford mpaka fedha hizo zitakapolipwa.

Pia, aliamuru mwanasheria wa kampuni hiyo, Edward Mroso awekwe mahabusu kwa saa 48 kisha aripoti ofisini kwake kueleza jinsi atakavyolipa fedha hizo.

Ingawa jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe hakumtaja DC huyo alipozungumza na waandishi wa habari, alitolea mfano wa mkuu wa wilaya aliyekadiria kodi kwa mwekezaji aliyebaini kuwa halipi.

Alisema zipo sheria na taratibu za kufuata na pia zipo mamlaka ambazo zinahusika moja kwa moja na uwekezaji.

Aliwataka viongozi kuwasiliana na mamlaka husika pindi kunapotokea tatizo.

“Kama mwekezaji ana tatizo lolote; diwani, mkurugenzi, DC au waziri awasiliane na sisi moja kwa moja ili tutatue tatizo hilo. Imejitokeza DC anakadiria kodi anavyoona yeye na kutaka kodi ilipwe ndani ya siku mbili. Sheria haisemi hivyo, hiyo si spirit ya Rais Magufuli ya kujenga nchi ya viwanda,” alisema Mwambe.

Alisema, “Zipo sheria ambazo zinatoa mwongozo kwenye masuala ya uwekezaji, kama ni suala la kodi, ipo Tax Administration Act (Sheria ya Usimamizi wa Kodi) ambayo kimsingi inasimamiwa na Wizara ya Fedha.”

Mwambe alisema TIC imejipanga kurahisisha mazingira ya uwekezaji nchini kupitia huduma za mahali pamoja na hivi karibuni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imejumuika na taasisi nyingine za Serikali zilizopo ndani ya TIC.

“Natoa wito kwa viongozi wote wa ngazi mbalimbali kuhakikisha tunashirikiana sawasawa kila mmoja katika taasisi yake. Tusiingiliane katika majukumu, kama ni vibali vya kuishi, kamishna wa Uhamiaji yupo, kama ni vibali vya kazi, kamishna wa kazi yupo,” alisema.

Alisisitiza, “Viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi na wananchi kwa jumla waishirikishe TIC pale wanaposhughulikia changamoto zinazohusiana na uwekezaji ili kituo kiweze kushauri vyema njia za kuzishughulikia.”

Mwambe aliitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuchunguza ili kuwabaini wawekezaji ambao hawajalipa kodi kwa zaidi ya miaka mitatu na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria akisema inashangaza kuona kampuni ambayo imefanya kazi kwa miaka saba nchini bila kulipa kodi yoyote wakati mamlaka hiyo ina ofisi kila mkoa.

“Nitamwandikia barua Kamishna wa TRA ili aweze kufuatilia maeneo yote ya uwekezaji ambayo hayajalipa kodi kuanzia miaka mitatu au zaidi. Haiwezekani kampuni inakaa miaka mitatu bila kulipa kodi mpaka inaondoka, wanakuja wawekezaji wengine ndio mnashtuka,” alisema.

Alipoulizwa kama TRA ina taarifa juu ya uwepo wa wawekezaji ambao hawalipi kodi, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo alikataa kuzungumzia suala hilo.

Alisema hawezi kuzungumzia walipa kodi waliotajwa na mkurugenzi wa TIC kwa kuwa hana taarifa zao za ndani.

Mwambe alizitaka kampuni ambazo hazijalipa kodi kufanya hivyo haraka kwa sababu ni wajibu wao.

Pia, aliitaka TRA kutimiza wajibu wake wa kuwafikia wawekezaji wote na kuwakadiria kodi stahili na kuhakikisha inalipwa.

Alisema uwekezaji ndiyo njia sahihi ya kufikia uchumi wa viwanda na ili kufikia lengo hilo, wana jukumu la kuijenga sekta binafsi kwani ndio nyenzo kuu.

Alichosema DC Ole Sabaya

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli hiyo ya TIC jana, Ole Sabaya alisema mtu yeyote anayekwepa kodi awe mgeni au mwenyeji ni mkwepaji kodi.

“TIC wanakubaliana na mimi kwamba hao wanaowaita wawekezaji hawajawahi kupewa cheti chochote cha kuwatambua,” alisema.

Alisema, “Makaratasi yaliyopo ofisini yalituonyesha kuwa hawa watu wamekwepa Sh713 milioni ila nilipowaelekeza TRA waniletee makadirio ya hao wanaoitwa wawekezaji wameleta jumla ya Sh1.6 bilioni na zaidi.”

Alisema msingi wa uwekezaji wenye tija ni ustawishaji wa uchumi wa nchi kwa kulipa kodi.

“Kodi ikishindikana kulipwa tena kwa mauzo ya hisa kwa njia ya vificho napata shida kuwaita watu hao wawekezaji,” alisema.

Alisema wanahamasisha uwekezaji unaofuata sheria, utaratibu na sheria za nchi.

“TIC watumie muda huu wanaomtetea bwana huyo kumwambia tunataka alipe kodi ya Serikali,” alisema.

Nyongeza na Mussa Juma

Chanzo: mwananchi.co.tz