Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TIC wapewa majukumu mazito uwekezaji

Uwekezaji Mafuta Mafta TIC wapewa majukumu mazito uwekezaji

Wed, 1 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amewataka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwatembelea wawekezaji kiliowasajili katika miradi yao ili kuona wanachokifanya na kuwasaidia wanapokwama.

Chongolo ameyasema hayo jana Februari 28, 2023 wilaya ya Ikungi mkoani Singida alipotembelea mradi wa kilimo cha alizeti ulioanzishwa na mwekezaji kutoka Jordan, kampuni ya Alfardaws Investment Co. Ltd.

Akiwa katika shamba hilo, Chongolo alipokea changamoto za mwekezaji ikiwemo ya kubadilisha ardhi aliyopewa na kijiji cha Choda kutoka kuwa ardhi ya kijiji kuwa ardhi ya jumla ili atambulike kama mwekezaji mkubwa.

Akiwasilisha taarifa ya mwekezaji, Edwin Nambiza ambaye ni mkandarasi katika mradi huo, amesema mwekezaji alipewa ekari 1,700 za ardhi kwa ajili ya kufanya kilimo kikubwa cha alizeti ambacho kitaenda sambamba na uzalishaji wa mafuta.

Amesema wamebaini kwamba kuna upungufu wa mbegu sokoni, hivyo watafanya kazi pia ya kuzalisha mbegu kwa wingi, tayari mitambo ya uzalishaji imefika na yuko tayari kufanya kazi endapo atawezeshwa.

Amebainisha changamoto zinazomkabili kuwa ni kupata hati ya uwekezaji kutoka TIC, jambo ambalo ameambiwa na Serikali za Mitaa kwamba wamewasilisha nyaraka zote kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kukamilika kwa mchakato huo.

"Mahitaji ya ardhi kwa ajili ya kilimo ni ekari 6000 na mwekezaji yuko serious na kilimo hiki, tunaomba utusaidie tupate hati, lakini pia tupate umeme kwenye eneo letu la mradi," amesema Nambize.

Akizungumzia suala la kupatiwa hati, Chongolo ameshangazwa na mwekezaji huyo kucheleweshwa kupatiwa hati na TIC na pia kupelekewa umeme ili aanze mradi ambao utakuwa na faida kubwa kwa wananchi.

“Hatuwezi kuwa na namba za wawekezaji wakati hatujui huko wanafanya nini. Nadhani twende hatua ya pili, twende huko kwa wawekezaji tuone wanachokifanya," amesema Chongolo.

Ameitakaza pia Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kuona fursa katika mradi huo kwani utawasaidia kukusanya mapato makubwa lakini pia wananchi watajiingizia kipato kitakachoboresha maisha yao.

Ameahidi kushughulikia suala la umeme ndani ya mwezi mmoja ili mwekezaji huyo afikishiwe umeme. Ameitaka pia halmashauri kumtafutia mwekezaji huyo ardhi anayohitaji ili afanye uwekezaji mkubwa zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live