Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TIC ilivyomrejesha mwekezaji wa mabilioni

D00af0820da078be99267cc7a0c354d7 TIC ilivyomrejesha mwekezaji wa mabilioni

Tue, 2 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKATI akimwapisha Mkurugenzi mpya wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dk Maduhu Kazi Julai 16 mwaka jana, Rais John Magufuli alimuagiza kufuatilia wawekezaji ambao wamekuwa wakikumbana na vikwazo, hususani kuzungushwa na maofisa wa serikali, katika kupata vibali mbalimbali.

Rais alibainisha kuwa wapo wawekezaji kutoka nje ya nchi wenye lengo la kuwekeza nchini tena uwekezaji wa mabilioni ya pesa lakini wanakwamishwa na sababu ambazo nyingine siyo za msingi.

Rais Magufuli alitolea mfano wa kampuni ya Elsewed kutoka Misri inayotaka kuwekeza kwenye ujenzi wa kiwanda cha vifaa vya umeme kwa gharama ya Sh bilioni 100.

Tangu kutolewa kwa agizo hilo, TIC imekuwa ikikimbizana katika kuhakikisha mwekezaji huyo ambaye alikuwa ameshakata tamaa na kuondoka kwenda kuwekeza nchi nyingine kurudi nchini.

Dk Kazi anasema walikutana na mwekezaji huyo na kufanya naye mazungumzo ya uwekezaji wake kisha kumpatia vibali vyote vya uwekezaji vinavyotakiwa.

Anasema wakati wakiwa wanaendelea na majadiliano waliona kuwa mwekezaji ana uwezo wa kukifanya kiwanda hicho kuwa kiwanda kikubwa cha kuzalisha bidhaa za umeme zitakazouzwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutokea Tanzania. Baadhi ya bidhaa hizo ni mashine za kupozea umeme (transformer), nyanya za umeme pamoja na vipuli vingine vinavyohitajika kwenye sekta ya umeme.

Kwa sasa mwekezaji huyo ameshawekeza Dola za Marekani milioni 50 kwenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 120,000 lililopo Kigamboni.

Kama TIC ingezembea kuitekeleza kauli ya Rais Magufuli au kama Rais Magufuli asingeshtukia kuwepo kwa mwekezaji huyo aliyekuwa anaelekea kukataa tamaa, Tanzania isingenufaika na uwekezaji huo mkubwa kutoka Misri.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Elsewedy Ukanda wa Afrika Mashariki, Ibrahim Qamar, anasema baada ya mazungumzo na TIC na kufahamishwa undani kuhusiana na faida za uwekezaji hapa nchini, iliamua kuongeza kiwango chake cha uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa kituo chake kikubwa cha uwekezaji katika eneo hili la Mashariki mwa Afrika.

Anasema uwekezaji huo pia umetokana na sera nzuri za uwekezaji zilizopo hapa nchini ambazo ziliivutia kampuni hiyo kuwekeza tangu awali.

Hata hivyo, Qumar anakiri kwamba kulikuwa na changamoto zilizosababisha kampuni hiyo kutaka kuondoka, lakini serikali ya Rais Magufuli iliingilia kati na sasa wamerejea jumla na kuahidi kuongeza uwekezaji nchini.

Mbali na kusifia ushirikiano wanaoendelea kuupata kutoka TIC, anasema: “Kiwanda hiki kitazalisha bidhaa za umeme kwa nchi za Afrika Mashariki na baadae Afrika nzima. Vifaa vingi vya umeme vitakuwa vikizalishwa kwa teknolojia ya roboti.”

Katika kuhakikisha uwekezaji huo unawanufaisha watanzania, kampuni hiyo pia itajenga Chuo cha Ufundi umeme kwa ajili ya kuwanoa wafanyakazi watakaoajiriwa kiwandani hapa ili wamudu uzalishaji wa vifaa vya kisasa zaidi kwa kutumia hizo roboti.

Anasema kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha nyaya za umeme tani 15,000 kwa mwezi, mashine za kupozea umeme (transfoma) 400 kwa mwezi na bidhaa nyingine muhimu zinazohitajika kwenye sekta ya umeme.

Kwa kuwa sera ya uwekezaji imelenga zaidi kuwanufaisha watanzania wa ngazi zote, kiwanda hicho kitaajiri wafanyakazi zaidi ya 400 ambapo kitaanza na wafanyakazi 250 kisha kuongeza wengine zaidi hadi kufikia wafanyakazi 400.

Kwa sasa anasema kiwanda kimefikia hatua ya ujenzi wa majengo na kimeshaagiza kusimika mashine zitakazotumiwa kuzalisha vifaa hivyo.

Dk Kazi anaongeza kuwa kituo hicho kimejipanga kufanikisha uwekezaji wa mwekezaji yoyote yule kwa uharaka na umakini wa hali ya juu hasa kwa kuzingatia kuhusu mchango muhimu wa uwekezji katika kuinua uchumi wa nchi.

Anasema kama mwekezaji huyo angeondoka ni wazi kuwa ajira, fedha na faida za uwekezaji wake ungeenda kunufaisha nchini nyingine na kwamba TIC itahakikisha kuwa inawavutia na kuwasaidia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kufanya uwekezaji wao nchini bila vikwazo.

“Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji kama madini, nishati, kilimo na maeneo mengine mengi. Kituo chetu kitashirikiana na kila mwekezaji mwenye nia nzuri ya kuchangia maendeleo ya nchi bila kumkwamisha,” anasema.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Tito Mwinuka, anasema uwekezaji wa kampuni hiyo hapa nchini utachagiza maendeleo ya miradi mbalimbali ya umeme nchini kufanyika kwa ufanisi na kwa gharama nafuu kwa kuwa bidhaa nyingi zitakuwa zikipatikana hapa nchini.

Anasema kutokana na fursa nyingi za masoko ya bidhaa za umeme kama hizo zitakazozalishwa kiwandani hapo, kampuni hiyo itapata faida kwa kuwa zitauzwa hata kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Anasema Tanesco imewaunganishia umeme wateja wengi zaidi kwa kipindi cha miezi sita ya mwaka huu na hiyo inatokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na wawekezaji wa ndani na nje katika kuzalisha biadhaa na vipuli na mashine kadhaa za kuzalishia umeme,

Kwa sasa anasema shirika haliagizi transfoma nje ya nchi wala nguzo au bidhaa nyingine za kuzalishia umeme kutoka nje ya nchi kwa kuwa bidhaa hizo zote zinapatikana hapa nchini.

Tangu serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani imekuwa mstari wa mbele kupigania ukuaji wa uchumi huku akiamini kuwa nchi inaweza kusonga mbele kwa kutegemea maendeleo ya viwanda na amekuwa akiwasisitiza wawekezaji wa ndani na nje ya kufanya uwekezaji wenye tija kwa taifa.

Rais amekuwa akisisitizia uwekezaji ambao utasaidia ajira kwa watanzania wa ngazi zote kuanzia wenye ujuzi na hata wasio na ujuzi. Amekuwa akiweka angalizo kwamba uwekezaji uwe unaolenga pande zote kunifaika, yaani nchi na mwekezaji na siyo uwekezaji wa kiujanjaujanja.

Chanzo: habarileo.co.tz