Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imefanya marejeo ya bei za mbolea ya UREA na DAP kulingana na gharama za kuingiza mbolea hiyo nchini. Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk Stephan Ngailo, kupitia taarifa yake kwa umma.
Dk Ngailo alisema bei hizo elekezi zilianza kutumika kuanzia jana kwa kampuni zote hadi hapo itakapotangazwa bei nyingine. Alisema kwa kuwa bei zilizotangazwa ni elekezi, hivyo wafanyabiashara wanaweza kuuza chini ya bei elekezi kulingana na biashara ya ushindani na kinyume chake ni kosa kisheria kuuza mbolea kwa bei ya juu ya bei elekezi kwa lengo la kujiongezea kipato.
“Ni muhimu kwa mamlaka zote ngazi za mikoa, wilaya na halmashauri kuhakikisha kuwa kila duka la pembejeo linabandika bei elekezi sehemu zinazoonekana kwa urahisi kwa wanunuzi,” alieleza Dk Ngailo.