Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TFRA yaonya wauzaji mbolea

158e535aa459a911bf37499405e4946c TFRA yaonya wauzaji mbolea

Tue, 22 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeagiza wauzaji mbolea zenye bei elekezi wazingatie bei zilizopangwa na serikali.

Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk Stephen Ngailo jana ilieleza kuwa wauzaji watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni ya kufanya biashara ya mbolea.

TFRA jana ilitangaza bei elekezi ya rejareja na jumla kwa aina nne za mbolea ikiwemo DAP, Urea, CAN na SA.

Ngailo alieleza kuwa bei elekezi hizo zimeanza kutumika jana nchi nzima na kwamba, uamuzi huo ni kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea ya Mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea za mwaka 2011 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017.

Dk Ngailo alisema kutokana na hali ya kupanda kusiko kwa kawaida kwa bei za mbolea katika soko la dunia, serikali kupitia Waziri wa Kilimo ilisitisha matumizi ya mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja na upangaji wa bei elekezi mwezi Julai, 2021.

Alisema hivi karibuni ilijitokeza changamoto ya baadhi ya kampuni kupandisha bei za mbolea bila sababu za msingi na hivyo kusababisha usumbufu kwa wakulima.

Alieleza kuwa, TFRA kwa kushirikisha kampuni zinazoingiza mbolea nchini imepanga viwango vya bei za jumla na rejareja kwa mbolea ili kuondoa uwezekano wa wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia changamoto zilizopo kwenye soko la dunia kujinufaisha kwa kupandisha bei kiholela na kuwanyonya wakulima.

Kuhusu mchanganuo wa bei, Dk Ngailo alisema viwango vya bei elekezi katika maghala ya Dar es Salaam itakuwa Urea mfuko wa Kg 50 itauzwa kati ya shilingi 104,000 – 106,000, aina ya DAP itauzwa kati ya shilingi 99,000 – 104,000, mbolea ya CAN itauzwa kati ya shilingi 80,000 – 85,000 na aina ya SA itauzwa kati ya shilingi 65,000 – 67,000.

Alisema viwango vya bei elekezi kwa rejareja vitatofautiana kulingana na umbali wa eneo kama ifuatavyo; - Urea ni shilingi 106,143 – 108,183 kwa mfuko wa kilo 50 katika Mkoa wa Dar es Salaam na shilingi 119,455 – 121,455 katika Halmashauri ya Karagwe mkoani Kagera.

DAP ni shilingi 101,042 – 106,144 mkoani Dar es Salaam na shilingi 114,252 – 119,456 katika Halmashauri ya Karagwe mkoani Kagera; CAN ni shilingi 81,663 – 86,762 katika Mkoa wa Dar es Salaam na shilingi 94,055 - 99,277 katika Halmashauri ya Karagwe Mkoa wa Kagera.

Mbolea aina ya SA ni shilingi 66,365 – 68,405 katika Mkoa wa Dar es Salaam na shilingi 78,112 - 80,163 katika Halmashauri ya Karagwe mkoani Kagera.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live