Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TCRA yawakomalia watoa huduma ving’amuzi vilivyozuiwa

16025 Tcra+pic TanzaniaWeb

Fri, 7 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikiendelea na mchakato wa fidia kwa watumiaji wa ving’amuzi vilivyozuiwa kuonyesha chaneli za ndani, imewataka watumiaji wa Azam Tv, Zuku na Dstv kuandika barua au barua pepe iwapo walitakiwa kulipia kifurushi chochote ili kuona chaneli ambazo zinatakiwa kuonyeshwa bure (FTA).

Agosti 7,2018  TCRA ilitangaza kusudio lake la kusimamisha leseni ya kampuni ya Multichoice Tanzania wamiliki wa king’amuzi cha DSTV na Simbanet Tanzania Limited inayomiliki Zuku kwa kuonyesha chaneli za ndani kinyume na matakwa ya leseni zao.

FTA inajumisha chaneli zote za ndani ambazo kabla ya kuingia katika mfumo wa dijitali zilikuwa zikitumia mkonga wa ardhini ambazo ni TBC1, ITV, Channel Ten, Eatv, Clouds na Star Tv.

Baada ya tangazo la TCRA watoa huduma wa ving’amuzi walianza kuziondoa chaneli hizo katika orodha ya chaneli zao licha ya kuwa tayari walifungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo.

Leo Septemba 6, 2018 TCRA imetoa tangazo katika gazeti la Mwananchi  ikitoa wito kwa wananchi kuandika barua au barua pepe endapo walitozwa gharama yoyote ili kuziona chaneli hizo wakati ambapo zilikuwa bado hazijaondolewa katika ving’amuzi hivyo.

“Kila aliyekuwa anatozwa kutazama chaneli za televisheni za TBC1, ITV, Star Tv, Channel Ten, EATV na Clouds Tv kupitia kisumbuzi (king’amuzi) kimojawapo kati ya Dstv, Zuku na Azam Tv atume taarifa ya jina lake kamili, aina ya kisumbuzi, namba ya kisumbuzi, eneo alilopo, kiasi cha pesa kwa mwezi na idadi ya miezi aliyolipia,” lilieleza tangazo hilo ambalo lilionyesha kuwa limetolewa na mkurugenzi mkuu wa TCRA.

Tangazo hilo limeeleza kuwa taarifa hizo zitatakiwa kutumwa katika barua pepe ya [email protected] au sanduku la Posta namba 474,14414 Dar es Salaam.

Hivi karibuni, Mwananchi digital ilifanya mahojiano na mkuu wa idara ya leseni wa TCRA, Andrew Kisaka aliyesema inakamilisha utaratibu wa kuanza kutoa fidia kwa watumiaji wa ving’amuzi kutokana na usumbufu walioupata kutoka kwa watoa huduma ambao hawakufuata masharti ya leseni zao.

“Tulikuwa tunasubili utulivu wa soko baada ya mambo haya yote yaliyopita, Septemba 5 soko litakuwa limetulia na tutakamilisha mchakato wa fidia. Fidia zitatolewa kwa mfumo wa huduma na siyo fedha taslimu watu wasije wakamalizana,” alisema Kisaka.

Alisema fidia hazitatolewa na watoa huduma ambao wamezuiwa kuonyesha chaneli hizo pekee, bali hata kundi la wale ambao walitakiwa kuonyesha bure lakini hawakufanya hivyo.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz